
JAJI wa shirikisho nchini Marekani, jana (Ijumaa) alitupilia mbali maombi ya mjumbe wa Baraza la Congress kutoka chama cha Republican yaliyotaka kumruhusu Makamu wa Rais, Mike Pnce, kuzipinga kura za majimbo maalum zilizopigwa kwa Joe Bidden wakati Baraza la Congress litakapokutana Januari 6, 2021, ili kuhalalisha alichokiita ushindi wa Rais Donald Trump.
Jitihada hizo za karibuni za wafuasi wa chama cha Republican kumtetea Trump ili kubadilisha matokeo ya uchaguzi uliofanywa Novemba 3, 2020, zilipingwa na mmoja wa maofisa wa Trump mwenyewe aitwaye Jeremy Kernodle aliyesema Mwakilishi Ooui Gohmert wa Texas na wapiga kura wa Republican katika jimbo la Arizona hawakubaliani na madai ya Pence na hivyo madai hayo hayana msingi.
Trump amekataa kukubali kushindwa na Biden na mara nyingi amedai uchaguzi ulitawaliwa na wizi wa kura ambapo yeye na wafuasi wake wamekwama katika madai yao kibao ya kutaka kubadilishwa kwa matokeo ya uchaguzi huo.
Biden alimshinda Rais Donald Trump kwa tofauti ya kura 306-232 katika majimbo maalum nchini humo, na anatarajiwa kuapishwa Januari, 20, mwaka huu.
Chini ya mfumo maalum wa kura za majimbo (Electoral College) kura hizo huhesabiwa kutokana na wingi wa watu katika majimbo likiwemo Jimbo la Columbia (DC) kufuatana na idadi ya uwakilishi wa Baraza la Congaress.