
MAPEMA tu, ameanza maajabu yake! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia mrembo anayefanya muziki wa Bongo Fleva, Zuhura Othman ‘Zuchu’ kuanza makeke yake kwa Mwaka 2021.
Katika ripoti mbalimbali za wasanii watakaotisha na kutazamwa zaidi barani Afrika, jina la Zuchu kutoka nchini Tanzania limetamalaki kila mahali.
Ripoti mbalimbali zinamuonesha Zuchu kwenye namba moja kisha wanafuata wengine kutoka nchi mbalimbali barani Afrika; kama ifuatavyo;
ZUCHU ripoti hizo zinamtaja Zuchu kama mwanamuziki anayechipukia ambaye ukuaji wake unashangaza.
Zuchu anaimba kwa lugha za Kiswahili na Kingereza na ana sifa zote za msanii wa Bongo Fleva.
Mara tu baada ya kusainiwa kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), mwaka jana, Zuchu aliachia EP (Extended Play) yake ya I AM Zuchu.
Kwa mujibu wa mitandao mbalimbali ya kusikiliza, kutazama, kupakua na kuuza muziki, EP hiyo ya Zuchu iliongoza kusikilizwa na video za muziki wake zimefanikiwa kutazamwa na mamilioni ya mashabiki kwenye Mtandao wa YouTube.
FIK FAMEICA
Mwingine ni Fik Fameica wa Uganda ambaye anajulikana pia kwa jina la Fresh Boy. Ni miongoni mwa wasanii wa rap waliovutia wengi kutoka Afrika Mashariki.
Mara ya kwanza jamaa huyo alipanda stejini mwaka 2017 akicheza kisha muziki wake ukaanza kutamba.
Kijana huyo hapigi muziki kama ule unaochezwa na wasanii wengine nchini Uganda kwani yeye hupiga muziki ambao umechanganyikana na rege.
Tayari jamaa huyo amefanya kolabo na wanamuziki maarufu kutoka kote Afrika akiwemo Patoranking, Vanessa Mdee na Joe Boy.
GAZ MAWETE
Gaz Mawete kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alianza muziki mwaka 2018.
Msanii huyo ambaye alijipatia umaarufu baada ya kushiriki mashindano ya kusaka vipaji, tayari amefanya kolabo na Fally Ipupa ambaye alionekana katika Wimbo wa C’est Rate.
Mawete pia alishiriki kwenye Albam ya Dadju Poison au Antidote.
Mawete ameongeza umaarufu wake baada ya kuteuliwa mwaka uliopita katika orodha ya Best African Act katika tuzo za muziki za MTV barani Ulaya.
KABZA DE SMALL
Kabza De Small wa Afrika Kusini amevutia wengi tangu alipoanza muziki 2016.
DJ huyo amepewa jina la utani la kuwa Mfalme wa Amapiano; aina moja ya muziki nchini Afrika Kusini.
Muziki wake ni wa kupendeza, wenye nguvu na kuvutia. Kabza De Small amekuwa bingwa wa sauti ambayo inapita katika nchi zingine za Kiafrika na imeanza kukubalika kote ulimwenguni.
Ushawishi wake unaweza kusikika katika nyimbo zilizorekodiwa barani kote na hiyo ilitambuliwa wakati alipochaguliwa katika Kipengele cha Best African Act katika Tuzo za MTV, mwaka uliopita.
KIDI
KiDi wa Ghana ni sehemu ya kizazi kipya cha wasanii wa Ghana ambaye alipata mafanikio wakati wimbo wake wa Sugar uliposhinda albam ya mwaka katika tuzo za muziki za Ghana 2020.
Muziki wa msanii huyo uliochanganyika na midundo ya Afrika unamfanya kuwa mwanamuziki ambaye muziki wake unaweza kusikilizwa na watu walio nje ya mipaka ya Ghana.
Mwaka jana wimbo wa KiDi Say Cheese ulimpa umaarufu wa kimataifa baada ya msanii wa Marekani, Teddy Riley kushirikiana naye kwenye Remix ya wimbo huo.
Kijana huyo pia ameshirikiana na wasanii wengine wa Afrika Magharibi wakiwemo Davido na Mr Eazi.
OMAH LAY
Omah Lay wa Nigeria ni chipukizi mwingine ambaye amepata umaarufu kupitia wimbo wake wa Bad Influence.
Kwa sauti yake ya kupendeza, msanii huyo anayekua haraka amejiweka kama mtu wa kutazamwa zaidi kwa mwaka 2021.
Mwaka jana, Omah Lay alipata matatizo baada ya kuzuiliwa nchini Uganda kwa madai ya kuvunja kanuni za Virusi vya Corona, lakini kampeni kubwa ya mitandao ya kijamii ya kuachiliwa kwake ilizidi kumpa umaarufu.
SHA SHA
Sha Sha ni mwimbaji kutoka Zimbabwe aliyejaaliwa sauti ambayo ilijionesha kwenye albam yake ya Blossom ya 2019.
Sha Sha ameorodheshwa kama mmoja wa wasanii 10 bora wa kike kwenye Mtandao wa Spotify huko Afrika Kusini.
Mwaka jana pia alishinda Kipengele cha Best International Act katika Tuzo za BET.
SORAIA RAMOS
Kwa kutumia sauti yake nzuri, Soraia Ramos wa Cape Verde anaimba masuala ya mapenzi kwa lugha ya Kireno na wakati mwingine Creole.
Mwimbaji huyo kwa sasa anapasua anga na wimbo wake wa O Nosso Amor aliomshirikisha Calema pamoja na Remix ya Wimbo wa Bai alioimba na Lisandro.
Kwenye Mtandao wa YouTube video zake zina maoni zaidi ya milioni 15.
TEMS
Listi hiyo pia inamtaja Tems wa Nigeria ambaye amewavutia mashabiki wake na wimbo wake wa Try Me aliouachia mwaka 2019.
Anafahamika kwa sauti yake ya kuvutia na muziki unaojumuisha miondoko ya soul, Hip-Hop na RnB.
Baada ya kuachia EP yake ya Broken Ears, anaendelea kuvutia mashabiki wake ndani na nje ya Nigeria.
ELAINE
Elaine wa Afrika Kusini naye anakuja kwa kasi akibebwa na sauti yake ya dhahabu.
Kusainiwa kwake chini ya lebo ya muziki ya Marekani ya Columbia, mwezi Agosti, mwaka jana, kumemwezesha kujenga msingi imara.
Elaine alitisha mwaka 2019 alipoachia wimbo wake wa You’re The One.
Wimbo huo ulimfanya kuwa mmoja wa wasanii wanaotazamwa zaidi nchini Afrika Kusini.
STORI; MWANDISHI WETU NA MTANDAO