
SERIKALI ya Tanzania kupitia Shirika la Reli (TRC) na China zimeingia makubaliano ya kujenga reli ya kisasa ya kilomita 341 kutoka Mwanza hadi Isaka. Mradi wa ujenzi huo wa Tsh. trilioni 3.0677 ulitangazwa kwa utaratibu wa zabuni, na kampuni ya China ilishinda.
Hicho ni kipande cha tano, ambapo kipande cha kwanza ni kutoka Dar mpaka Morogoro, cha pili ni kutoka Morogoro hadi Makutupora. Mkataba wake umetiwa saini mbele ya Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.
Akizungumza katika hafla hiyo, Magufuli amewashukuru na kuipongeza kampuni ya Kichina iliyoshinda tenda ya kujenga KM 341 za ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mwanza hadi Isaka na kuongeza kuwa ana matumaini kwamba watafanya kazi kwa uadilifu.
“Ujumbe kutoka kwa Rais wa China Xi Jinping, tumeupokea lakini na mimi nimetuma ujumbe mwingine umfikishie Rais wa China na mimi mambo niliyomueleza ni masuala ya kushirikiana kwa hizi nchi mbili katika masuala ya kiuchumi.
“Kwa ujumla mazungumzo tuliyoyafanya yalikuwa mazuri na nimemhakikishia Tanzania itaendelea kushirikiana na China kwa sababu ni ndugu zetu, sasa ni wakati wa Tanzania na China kujenga uchumi kwa nguvu zote na kuonyesha ushirikiano mkubwa,” amesema Magufuli.
Aidha, Waziri wa mambo ya Nje wa China, Wang Yi, ameyaagiza makampuni ya China yanayotekeleza miradi hapa Tanzania kutekeleza miradi hiyo kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania.
Pamoja na ushirikiano uliopo kwenye sekta nyingine ikiwemo sekta ya miundombinu, uhusiano baina ya Tanzania na China umezidi kuimarika zaidi katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama). Kupitia kampuni ya Huawei, China imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika kufanikisha miradi mbalimbali inayolenga kuboresha sekta ya Tehama sambamba na kukuza na kuibua vipaji vya sekta hiyo muhimu hapa nchini.
Matunda ya ushirikiano huo yalijidhihirisha hivi karibuni ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alikabidhi tuzo kwa washindi washindano la Tehama duniani lililoandaliwa na kampuni ya Huawei ambapo wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walishika nafasi ya pili ulimwenguni.