×

Asakwa Tuhuma za Kumnyonga Mchumba’ke

PENZI la kifo! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia kijana Yusuf Ally (25), mkazi wa Kijiji cha Msimbo Kata ya Msimbi wilayani Kisarawe, Pwani, kusakwa kwa tuhuma za kumnyonga mchumba’ke, Rehema Khamis hadi kifo.

 

Tukio hilo la kusikitisha lilijiri kwenye kijiji hicho siku ya Sikukuu ya Krismasi ambapo kuliibuka taharuki kubwa.

Akizungumza na Gazeti la UWAZI kwa masikitiko makubwa, mama wa marehemu, Sikujua Khamis alisema kuwa, hakutegemea kama kijana mdogo kama Yusuf angehusika na ukatili kama huo.

 

“Yusuf ni kijana ambaye ninafahamu, amekuwa kwenye uhusiano wa mapenzi na mwanangu kwa miaka mitatu.

“Alikuwa akikaa hapahapa kwangu wiki mbili au tatu kisha anarudi kwao.

“Hata mchumba’ke (Rehema) alikuwa akienda naye kwao.

“Siku ya tukio, asubuhi tuliamkia shambani mimi na mume wangu, tulirudi mchana saa sita.

“Hatukujua chochote, baada ya muda, nikiwa ninaandaa mboga ndipo akaja mdogo wangu, akanipa taarifa mbaya zilizonishtua.

“Kwa kweli nilishtuka na sina cha kufanya kwa sababu asubuhi niliwaacha wakiwa wamelala ndani.

“Basi, baada ya hapo ndipo tukaanza kuuliza kilichotokea na kiukweli sikuwahi kuona wana tofauti yoyote,” alisema mama huyo kwa uchungu.

 

Kwa upande wake mdogo wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Arafat, naye alisimulia;

“Asubuhi mimi niliamka, nikiwa naokota maembe, mara akapita dada na shemeji (Yusuf na Rehema) wakisema wanakwenda shamba, lakini hawakufika mbali, nikasikia dada akipiga kelele akisema; ‘Yusuf niache!’

“Sikufuatilia, lakini baada ya muda, Yusuf alinifuata akanituma diclopar ya shilingi 600 na diclofenac ya shilingi 400 (hizi ni dawa), nikaenda kununua.

 

“Nilipomrudishia, nilimuuliza dada yuko wapi? Akasema anaoga, basi sikujua kinachoendelea mpaka watu walipojaa na baadaye kumkuta dada amefariki dunia kwa kunyongwa,” alisema mdogo wa marehemu.

 

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Msimbo, Jabir Bahatisha Sultani alisema kuwa, Disemba 25, mwaka jana ilikuwa Sikukuu ya Krismasi ambapo alipokea taarifa za kijana Yusuf kudaiwa kumnyonga Rehema.

 

“Baada ya tukio hilo niliambiwa Yusuf alikimbilia kwa rafiki yake kumueleza kuhusu kifo cha Rehema na yeye kujaribu kujiua bila mafanikio hivyo akawa anaomba akanunuliwe sumu kwani naye hataki kuishi.

 

“Baada ya kumueleza maneno hayo, rafiki yake akamwambia amsubiri akamletee hiyo sumu ndipo rafiki yake huyo akaenda kutoa taarifa kwa mjumbe aitwaye Hamis Chamwiti.

 

“Baada ya kupewa taarifa, mjumbe alinipigia mimi na kumpigia Diwani Mbegu Salum Lwambo, ikabidi wote tuwahi eneo la tukio.

“Diwani alitoa taarifa kituo cha Polisi cha Kisarawe, lakini mgambo wa kijiji walifika na katika kutafutatafuta mashambani ndipo tukaukuta mwili wa marehemu.

 

“Baada ya hapo ilibidi taratibu nyingine zifuate na tuliporudi kule alikokuwa mtuhumiwa hatukumkuta hivyo taarifa zake zipo Polisi na anaendelea kusakwa ili akajibu tuhuma za mauaji zinazomkabili,” alisema.

 

CHANZO CHA KIFO CHATAJWA

Aidha, Mwenyekiti huyo aliendelea kufafanua kuwa alizungumza na wazazi wa marehemu kutaka kujua kama kulikuwa na tatizo wanalolijua.

 

“Kwa mujibu wa wazazi wa marehemu, mtuhumiwa na marehemu wamedumu kwenye mahusiano kwa miaka mitatu lakini miezi miwili iliyopita marehemu alimwambia mchumba wake kuwa kama hayupo tayari kufuata taratibu za kuingia kwenye ndoa basi waachane.

 

“Baada ya maneno hayo mwanaume akaondoka akarudi kwao huko kijiji cha Mtamba kata ya Masaki na Disemba 23, 2020 akarudi na kumueleza mchumba wake kuwa nimerudi kamili kuanza taratibu za ndoa basi na baba anakuja kuleta mahari matokeo yake ndio tukio likatokea,” alisema.

HABARI; AISHA HUSSEN, PWANI

Leave a Comment