×

Matatani Kunywa Pombe na Wanawake Wawili Baa

KWANI kunywa bia na wanawake wawili baa ni kosa kisheria? Si ndivyo utakavyohoji?

Sasa UWAZI linakuambia wewe endelea na udadisi wako na uthubutu kufanya hivyo kizembe yakukute yaliyomkuta jamaa mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Michael (47) aliyejikuta matatani kwa kujiachia na wanawake wawili usiku wa mkesha wa Sikukuu ya Krismas.

 

ILIKUWAJE?

Desemba 22, 2020, Michael ambaye anafanya kazi ya uhandisi wa visima mkoani Tanga ingawa ni mwenyeji wa Moshi mkoani Kilimanjaro, alirejea kwao kwa ajili ya mapumziko ambapo inadaiwa alifikia kwenye hoteli moja mjini Moshi (jina linahifadhiwa) kwa ajili ya kujipumzisha kabla ya kuendelea na safari kuelekea kijijini kwao.

Baada ya kuhifadhi vyema vitu vyake chumbani, mhandisi huyo aliamua kutoka kwenda kupunguza uchovu wa safari kwa kupata bia mbilitatu kwenye eneo moja maarufu mjini Moshi.

 

Kinyume na maratajio yake ya kustarehesha mwili, Desemba 24, mwaka jana wakati sherehe ya Krismas ikiwa imepamba moto Michael alijikuta akiwa hoi chumbani kwake alikokuwa amefikia.

Baada ya kupata fahamu kidogo na kukagua vitu vyake alijikuta akiwa ameibiwa kila kitu.

 

Kufuatia hali hiyo aliamua kuwaita wahudumu wa hoteli hiyo na kuwaomba simu ili awasiliane na rafiki yake ili aje aokoe jahazi maana tayari maji yalikuwa yamezidi unga.

Kwa mujibu wa maelezo aliyotoa polisi Michael anasema rafiki yake ndiye aliyemsaidia kumpeleka polisi na kisha baadaye katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi kwa ajili ya matibabu.

 

MUDA WA KUKUMBUKA UKAWADIA

Baada ya kujiuliza kwa kina “nini kimemtokea?” Ndipo alipoanza kupata kumbukumbu kuwa jana yake baada ya kuweka vitu vyake sawa chumbani alitoka hotelini hapo na kwenda kupata bia mbilitatu sehemu moja maarufu mjini Moshi.

 

Anasema akiwa huko alikutana na wanawake wawili ‘pisi kali’ kwa msemo wa vijana wa kileo ambao walimuomba kwa unyenyekevu kampani yake ambapo naye bila hiyana aliwaambia “karibuni.”

Akizungumza kwa shida akiwa hospitalini alikokuwa akipatiwa matibabu Michael anasema wanawake hao walijitambulisha kwake kuwa wanafanyakazi Hospital ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, jambo ambalo siyo la kweli.

 

“Nilikunywa nao hadi muda fulani hivi usiku, nikaamua niwaage ili nirudi hotelini nilikokuwa nimefikia.

“Nao wakasema wanaondoka na hivyo kutaka niwape lifti ambapo niliondoka nao hadi nilipokuwa nimefikia nako tukaendelea kunywa.

“Kilichotokea sifahamu lakini nimeamka asubuhi niko chumbani na kila kitu kimeibwa,” alisema Michael.

 

TAARIFA KUTOKA HOSPITALINI

Taarifa na vipimo kutoka hospitalini zinasema kuwa Michael alifikishwa pale akiwa kwenye hali dhoofu ambapo alipokelewa kwenye kitengo cha dharura saa 8:30 mchana.

 

“Tulimwekea dripu ya maji ili kuondoa huo uchovu unaomfanya asijitambue vizuri.

“Kinachoonekana ni kwamba alinyweshwa vidonge vya usingizi maana ingekuwa sumu tungeona dalili nyingine za hatari,” alisema daktari wa zamu ambaye hakutaka jina lake litajwe.

 

POLISI WAONYA

Mbali na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Emmanuel Lukula kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea kufanya uchunguzi, amekemea tabia ya watu kuwakaribisha wageni ambao hawawafahamu na kushirikiana nao kwenye mambo ya jamii ikiwemo kushiriki vinywaji na chakula.

 

“Ni tabia hatarishi, ni vyema watu wakachukua tahadhari za kujilinda, huwezi kukutana na watu ghafla na kuanza kushirikiana nao kula na kunywa kilevi,” alisema Lukula.

Aliongeza kusema kuwa suala la ulinzi linaanzia kwa mtu husika kabla ya kushirikisha vyombo vya usalama kama polisi.

HABARI; MWANDISHI WETU, MOSHI

Leave a Comment