×

Kisa Morrison, Yanga Yampa Mkataba Mgumu Fiston

UONGOZI wa Yanga umewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia kuwa wamempa mkataba mshambuliaji wao mpya Mrundi Fiston Abbdulrazack wenye manufaa kwa pande zote mbili.

 

Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni siku chache tangu mashabiki wa timu hiyo waingie hofu ya kuondoka nyota huyo kama alivyoondoka aliyekuwa kiungo wao Mghana Bernard Morrison kwenda Simba aliyesaini miezi sita sawa na atakaopewa Fiston.

 

Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), mchezaji anapokuwa na mkataba wa miezi sita anakuwa huru kufanya mazungumzo na klabu nyingine itakayomuhitaji kama ilivyokuwa kwa Morrison aliyetimkia Simba.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Haji Mfikirwa alisema kuwa katika mkataba wao wa miezi walioingia na Fiston una vipengele mbalimbali ikiwemo kuongeza mwingine mara baada ya huo alionao kumalizika.

Mfikirwa alisema kuwa mara baada ya mkataba wa miezi sita utakapomalizika, Yanga ndiyo watakaokuwa na maamuzi ya kumuachia kuondoka au aongeze mkataba mwingine tofauti na ulivyokuwa wa Morrison.

 

“Niwaondoe hofu mashabiki wa Yanga kwa kuwaambia kuwa Fiston ni mali yetu na hakitatokea kitu chochote kibaya, licha ya kusaini mkataba wa miezi sita kwani yapo makubaliano mazuri kutoka katika pande zote mbili kwa maana ya klabu na mchezaji mwenyewe.

 

“Hofu iliyokuwepo ni ya kuondoka kwenda kuichezea timu nyingine kutokana na muda mfupi wa miezi sita tuliompa katika mkataba wetu, hivyo Wanayanga waondoe hofu katika hilo kwani tunajua tunachokifanya uongozi.”

 

Katika hatua nyingine, Championi Jumatanolimepata taarifa kuwa mshambuliaji huyo anatarajiwa kutua nchini keshokutwa Ijumaa kwa ajili ya kusaini mkataba huo mpya mara baada ya kufikia makubaliano mazuri. Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuripoti kambini Januari 25, mwaka huu kwa ajili ya kuanza mazoezi baada ya kupewa mapumziko ya wiki moja.

Stori: WILBERT MOLANDI,Dar es Salaam

Leave a Comment