×

Shigongo Aendelea Kuwagusa Watoto Wasiojiweza

ZOEZI la kuwashika mkono watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo katika Jimbo la Buchosa limezidi kupamba moto kwenye shule za msingi mbalimbali zilizopo katika jimbo hilo.

 

Zoezi hilo leo limeendelea tena leo Ijumaa, Januari 22, 2021, katika Kata ya Kafunzo na Nyehunge ambapo jumla ya wanafunzi 2,475 wa darasa la kwanza katika shule hizo wamepatiwa madaftari pamoja na wanafunzi wengine wenye uhitaji ambao wamepatiwa madaftari na sare za shule ili waanze masomo yao.

 

Baadhi ya wazazi waliopata msaada huo unaotolewa na Mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Eric Shigongo wamesema kampeni iliyoanzishwa na mbunge wao imewahamasisha kupeleka watoto shule tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo wameahidi kumuunga mkono kwa kila hali ili kuhakikisa malengo yanafikiwa ya kuinua kiwango cha elimu katika Jimbo la Buchosa.

 

Aidha, wamesema wapo tayari kuchangia na kujitolea katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye maeneo yao ili kujiletea maendeleo na kuiletea maendeleo chanya Buchosa.

 

Mhe. Shigongo kupitia kampeni yake ya BUCHOSA MPYA, PELEKA MTOTO SHULE ameendelea kugawa sare za shule na madaftari kwa wanafunzi hao ambao wanatoka katima familia zisizo na uwezo ili kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto wao shule jambo ambalo pia aliliahidi wakati wa kampeni zake.

 

Mwakilishi wa Kamati ya Hamasa ya Buchosa Mpya, Charles Matiku amesema Mhe. Shigongo amedhamiria kuleta maendeleo ya kweli katika Jimbo la Buchosa ikiwa ni pamoja na kuinua kiwango cha elimu katika shule za msingi na sekondari jimboni humo.

 

 

Ameongeza kuwa wazazi wanao wajibu wa kuwapeleka watoto wao shule na kuwahimiza kusoma kwa bidi huku Serikali nayo ikifanya wajibu wake wa kupeleka miundombinu ya elimu na kuendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na kujifunzia.

 

Zoezi hilo litaendelea katika kata zote 21 na vijiji vyote 84 vya Jimbo la Buchosa mpaka pale watoto wote wenye uhitaji watakapopata mahitaji yote muhimu yatakayowawezesha kuanza/kuendelea na masomo yao.

 

 

 

 

 

 

PICHA: IDDI MUMBA 

STORI: EDWIN LINDEGE

Leave a Comment