
BILIONEA wa Kitanzania, Mohammed Dewji maarufu MO amefunguka juu ya kutajwa kwenye orodha ya mabilionea wanaoongoza kwa utajiri barani Afrika.
Katika orodha hiyo ya jarida mashuhuri la Forbes linalofuatilia utajiri wa watu, kwa mwaka huu limemtaja Mo mwenye umri wa miaka 45 kama bilionea namba 13 akitoka nafasi ya 17 mwaka jana huku mfanyabiashara wa saruji, sukari na unga (Aliko Dangote wa Nigeria) akiendelea kuongoza orodha hiyo kwa kushikilia namba moja.
Leo Jumapili, kupitia ukurasa rasmi wa Timu Simba ambayo yeye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi amenukuliwa; “Nawapenda Watanzania wenzangu na uwekezaji tulioufanya umesaidia wananchi wa nchi hii niipendayo sana.

“Kiukweli sijivunii utajiri bali najivunia kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Taifa langu zuri. Shukrani Serikali yangu chini ya jemedari wetu, Rais Dk John Magufuli Kwa kutuwekea mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yanatupa hiyo fursa ya kutambuliwa na majarida makubwa ulimwenguni kama Forbes. Shukrani Watanzania wenzangu.”
Mpaka sasa Mo Dewji ameajiri zaidi ya watu 33,000 kupitia kampuni yake ya @metlgroup.
Inaelezwa kuwa utajiri wa Mo wa sasa ni Dola za Marekani bilioni 1.6 (Sh3.7 trilioni) na anayeshikilia namba moja utajiri wake ni Dola 12.1 bilioni (Sh28.9 trilioni).
Katika orodha ya jarida hilo ya Januari mwaka jana, Mo anayefanya biashara mchanganyiko alikuwa nafasi ya 17 akiwa na utajiri huohuo wakati mwaka juzi alishika nafasi ya 14 akiwa na utajiri wa Dola bilioni 1.9.