
IKIWA ni siku chache tu tangu kutambulishwa kwake kama ndiye kocha mpya wa Simba, Mfaransa, Didier Gomes tayari ameanza kuutambulisha mfumo wake ndani ya klabu hiyo ambao anaamini utawapa mafanikio katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo mara baada ya kutambulishwa juzi Jumapili mchana, jioni yake alihudhuria katika mazoezi ya kwanza ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Simba Mo Arena jijini Dar na kupokewa kwa shangwe na mashabiki wa Simba ambao walionyesha mapema kumkubali.

Katika mazoezi hayo, yalihudhuriwa na wachezaji 13 tu wa Simba huku wachezaji wengine wakiwa bado hawajaripoti kambini kutokana na kuwa likizo, wengine wakiwa katika majukumu ya timu ya Taifa ya Tanzania inayoshiriki michuano ya CHAN.

Wachezaji waliohudhuria mazoezi hayo ni Thadeo Lwanga, Rally Bwalya, David Kameta, Perfect Chikwende, Miraji Athumani, Ibrahim Ajibu, Mzamiru Yassin, Kennedy Juma, Gadiel Michael, Chris Mugalu, Ally Salim, Bernard Morrison na Mohammed Hussein.
Katika mazoezi hayo ya juzi, Kocha Gomes alitumia takribani dakika 120 kuwafua wachezaji hao ambapo walitumia zaidi ya dakika 60 katika mazoezi magumu ikiwa pamoja na kukimbia kwa spidi jambo ambalo linaashiria kocha huyo anahitaji timu ipate ufi ti wa kupambana bila kuchoka.
Ukiachana na mazoezi ya ufi ti, pia kocha huyo alitumia zaidi ya dakika 40 za kuuchezea mpira pamoja na kutoa mazoezi ya mbinu zake ambapo alionekana kuhitaji timu yake iweze kukaba kuanzia juu ili kuwafanya wapinzani wapoteze mipira kisha wakiipata waweze kumiliki bila kupotea kirahisi.

Katika kuhakikisha kuwa wachezaji wamemuelewa kocha wao, Gomes aliweza kuwagawa wacheza sita katika makundi mawili na kutengeneza timu mbili ambazo zilitakiwa kucheza mpira kulingana na maelekezo yake huku wachezaji hao wakitakiwa kufunga mabao.
Makundi hayo mawili yalikuwa hivi; Rally Bwalya, Perfect Chikwende, David Kameta, Mohammed Hussein, Gadiel Michael na Chris Mugalu.Kundi lingine likiwa na Kennedy Juma, Thadeo Lwanga, Mzamiru Yassin, Miraji Athumani, Ibrahim Ajibu na Bernard Morrison.
Katika timu hizo mbili walitumia dakika 40 kucheza mechi mazoezi kwa kufuata mfumo wa kukabia juu wa Kocha Gomes ambapo walitumia dakika 20 kwa kipindi kimoja kisha kumalizia nyingine 20 kipindi cha pili.
Kocha huyo pia alitumia dakika 20 zilizobaki kwa ajili ya mazoezi ya viungo vya mwili huku akitumia nafasi hiyo kufanya nao mazoezi na kuwaelekeza namna ya kufanya mazoezi hayo jambo ambalo lilikuwa likishangiliwa na mashabiki wengi wa Simba ambao walionekana kumkubali.
Mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Kocha Gomes alisema ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha timu hiyo inakuwa fi ti kwa ajili ya michezo inayofuata ikiwemo michuano ya Simba Super Cup.
“Nimefurahi kuona mashabiki wa Simba wamejitokeza kwa wingi mazoezini na kunipokea vizuri, kuhusu timu bado inahitaji mazoezi ya kutosha ili iwe fi ti na ndiyo maana utaona kuwa nilitumia muda mwingi kuwapa mazoezi magumu ikiwepo pamoja na kukimbia kwa spidi.

“Timu yangu inahitaji kukaba kuanzia juu ili kuwafanya wapinzani wapoteze mipira kirahisi kisha sisi tuumiliki mpira, timu haiwezi kufanya hivyo kama haitakuwa na mazoezi ya kutosha,” alisema kocha huyo na kuongeza:“Nafurahi kuwa hapa, nimejifunza vitu vingi ndani ya muda mfupi, nimepata nafasi ya kufahamiana na baadhi ya wachezaji na kuanza maandalizi ya Simba Super Cup, hii ni michuano yetu hivyo tunapaswa kujiandaa vizuri ili kuhakikisha hatuwaangushi mashabiki wetu.
“Naamini hayatakuwa mashindano rahisi, lakini naamini tutafanya vizuri kwa kuwa natarajia wachezaji wangu wanajua ukubwa wa dhamana waliyopewa kwa kuvaa jezi ya Simba, hivyo nataka kuona kila mmoja anacheza kwa kiwango cha ubora wa Simba.
“Simba ni miongoni mwa klabu 16 bora barani Afrika na inaheshimika sana mbele ya wapinzani wake, hivyo nasi ni lazima tuhakikishe viwango vya wachezaji wetu vinaakisi ukubwa wa klabu hii, tuna malengo ya kufi ka mbali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kupanda juu zaidi kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (kwa sasa vinara ni Yanga huku Simba wakishika nafasi ya pili).
“Kwa sasa kiasi kikubwa cha mazoezi tutakayofanya ni yale ya kurejesha utimamu wa mwili kwa kuwa tuliwapa wachezaji wetu siku kumi za mapumziko kisha tutaanza mazoezi ya mbinu taratibu.”Katika michuano ya Simba Super Cup, Simba itapambana na Al Hilal na TP Mazembe, huku kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikipangwa Kundi A na timu za Al Ahly, AS Vita na Al Marreikh.
Kocha huyo wa zamani wa Al Marreikh, anapenda kutumia mfumo wa 4-2-3-1 akitumia mshambuliaji halisi mmoja, viungo washambuliaji watatu, viungo wakabaji wawili na mabeki wanne. Mfumo mwingine ni wa 4-4-2 ambao unamruhusu kutumia washambuliaji wawili, viungo wanne na mebeki wanne.
MTAMBO WA MABAO WATAMBULISHWA RASMI
Jana jioni, Simba ilimtambulisha mshambuliaji wao mpya, Junior Lokosa raia wa Nigeria ambaye aliwahi kuichezea Esperance ya Tunisia.Lokosa ambaye anatajwa kuwa mtambo wa mabao, jana jioni katika mazoezi ya timu hiyo, alifunga mabao mawili ya maana.Mshambuliaji huyo alitua nchini Jumamosi iliyopita, jana Jumatatu akatambulishwa rasmi.
WAANDISHI: SAID ALLY, WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA