
PAULINA DAUDI (30) mkazi wa Mtaa wa Mageuzi Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga ameuawa kwa kupigwa ngumi na mchi (mtwangio) na mmewe aitwaye Samwel James baada ya kutokea ugomvi wa kifamilia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea Jumanne Januari 26, 2021 majira ya saa tatu asubuhi na kutaja chanzo cha mauaji hayo kuwa ni ugomvi wa kifamilia.
“Paulina Daudi (30) mkazi wa Mageuzi alishambuliwa kwa kupigwa ngumi na mchi mdogo sehemu mbalimbali za mwili wake na mume wake aitwaye Samwel James akiwa nyumbani,” amesema Magiligimba.
Ameeleza kuwa Paulina Daudi alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga.
Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi za kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa kwa kosa la mauaji kwani alikimbia mara baada ya tukio hilo. Pia ametoa wito kwa wanandoa kuacha mara moja tabia ya kuwashambulia wenza wao.
Aidha amewasisitiza wanawake wote wanaofanyiwa vitendo vya ukatili mkoani Shinyanga wavunje ukimya, wafunguke ili matatizo yao ya kifamilia yaweze kushugulikiwa yakiwa katika hatua za awali kabla madhara makubwa hayajatokea, akibainisha kuwa vitendo vya ukatili ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine.