
RAIS John Magufuli, leo Februari 2, 2021, amemwapisha Jaji Zepharine Nyalugenda Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Jaji huyo aliteuliwa kushika wadhifa huo baada ya kuonyesha uzalendo kwa kuwa jaji wa kwanza kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili.
“Nakupongeza Jaji Galeba kwa kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa. Nilimteua Galeba kwa sababu pamoja na mambo mengine aliendesha kwa Kiswahili hukumu ya North Mara Gold Mining dhidi ya Gerald Zumbi katika kesi ya mapitio no. 23 ya mwaka 2020. Ni ushujaa na uzalendo.

“Mahakamani mshtaki na mshtakiwa wanaongea Kiswahili, mashahidi wanaongea Kiswahili, wazee wa mabaraza, jaji/hakimu wanaongea Kiswahili lakini ikifika wakati wa kuandika mwenendo wa kesi au hukumu, inaandikwa kwa Kiingereza. Hii inawanyima haki na kuwaongezea gharama wananchi.
“Naungana na wote waliotangulia kumpongeza jaji mpya wa Mahakama ya Rufaa, Jaji Galeba, kwa kuteuliwa kwake, kama jaji. Galeba nilimteua jana, pamoja na masuala mengine, nilimteua kwa sababu ya ujasiri wake wa kuandika hukumu kwa Lugha ya Kiswahili” amesema Magufuli.