
JEFF BEZOS ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Amazon, amejiuzulu katika wadhifa wake wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ya biashara ya mtandaoni ambapo nafasi yake sasa itachukuliwa na Andy Jassy, ambaye kwa sasa anaongoza biashara ya uhifadhi wa data.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 3, 2021, na Andy Jassy imeeleza kuwa Bezos atakuwa mwenyekiti wa kampuni hiyo na atashiriki kimamilifu katika shughuli zote za kuiongoza kampuni hiyo.
Aidha Jassy ameeleza kuwa mabadiliko hayo yatafanyika katika kipindi cha nusu ya pili cha mwaka 2021.
Jeff amekuwa Mtendaji mkuu wa kampuni (CEO) hiyo kwa miaka 27 na kufanikiwa kwenye biashara za mitandaoni huku ikitoa ajira kwa watu milioni 1.3 duniani.
Jarida la Forbes limetaja Bezos kama tajiri namba mbili duniani akiwa na utajiri wa Dola za Marekani bil. 182 sawa na Sh. Trilioni 422 za Tanzania.