×

TAMISEMI Kusaka Kodi Nyumba kwa Nyumba

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amesema kuanzia tarehe 15 hadi 28 Februari wataendesha kampeni ya kuorodhesha majengo yote nchini ili wamiliki wake waweze kulipa kodi.

 

Jafo amebainisha hayo leo mkoani Morogoro kwenye uzinduzi wa kiwanda cha kusindika mazao jamii ya kunde ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Dkt. John Magufuli.

 

Jafo ameongeza kuwa Watendaji wote wa Serikali za Mitaa na vijiji kuanza kupita nyumba kwa nyumba kuorodhesha majengo yote kuachilia majengo ya Tasisi za dini ili kuhakikisha Serikali inapata kodi kwa ajili ya mstakabali wa Taifa.

 

“Kwahiyo niwaombe watanzania kuanzia Jumatatu tunaanza kampeni itakayoisha tarehe 28 mwezi huu na mimi pamoja na watendaji wakuu wangu wote tutashiriki zoezi hili tunataka tuorodheshe majengo yote ndani ya Tanzania ukiachilia majengo ya dini ili tuweze kulipa kodi kwa mustakabali wa nchi yetu,” amesema Jafo.

 

 

Aidha, Waziri Jafo ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji ili kuwawezesha wawekezaji kuwekeza nchini kwa kuwa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha maeneo yanatengwa.

Leave a Comment