
RAIS John Magufuli amefanya uzinduzi wa daraja la juu la Ubungo lililopewa jina la aliyekuwa katibu mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi aliyefariki dunia Februari 17, 2021. Kiongozi mkuu huyo wa nchi amezindua barabara hiyo leo Jumatano Februari 24, 2020 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu jijini Dar es Salaam.
Amewasili eneo hilo saa 3:50 asubuhi na kufanya uzinduzi kwa kukata utepe na baadaye alikwenda kuvuta kamba na baada ya kumaliza alishuka eneo la chini la daraja hilo na kuzindua rasmi kwa kufunua jiwe la msingi lililowekwa eneo hilo.
Kabla ya kukata utepe mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Patrick Mfugale amesema Kijazi Interchange lina urefu wa mita 700 barabara ya kutoka Buguruni kwenda Mwenge na umbali wa mita 260 kutoka Kimara kwenda Manzese na kwamba barabara za chini zina umbali wa kilomita tano.
“Nimeona tuliite Daraja hili ‘Kijazi Interchange’, na naamini mtakubaliana na mimi, Eng. Kijazi amefanya kazi kubwa sana kwenye Sekta ya Barabara, alikuwa hana makuu, yeye ndiye alikuwa Mkurugenzi wa Barabara nchini alipotoka yeye akaja Mfugale kisha akaja Iyombe.
“Iyombe na Kijazi ambao walikuwa Wakurugenzi wa Barabara nchini, baadaye wote walikuwa Makatibu Wakuu, Mfugale yeye ameukosa Ukatibu Mkuu kwasababu hata umri sasa hivi hawezi kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu, ila Kijaz alifanya kazi kubwa.
“Sikusubiri kwa mujibu wa Sheria kumuacha Waziri au Wizara ya Ujenzi watangaze jina la Interchange hii nikaona niwahi niite Interchange hii jina la Kijazi maana najua atakayelifuta jina hili ni Rais atakayekuja naye nitamshangaa kwanini alifute jina hili,” Rais Magufuli.