
UKIMYA wa supastaa wa muziki anayefanya vizuri zaidi barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, umemponza na kumfanya ashambuliwe na baadhi ya mashabiki wake.
Diamond au Mondi amejikuta akishambuliwa kila kona kwa madai kwamba amekuwa kimya na kumuacha aliyekuwa msanii wake, Rajab Abdul ‘Harmonize’ kuendelea kutamba na kuishika mitandao ya kijamii na penzi lake jipya na mwigizaji Kajala Masanja.
Mbali na kumuacha Harmonize au Harmo kutamba na Kajala wake, pia ameshindwa kukimbizana naye kwa kutoa ngoma kali mfululizo.
Kadiri Harmo anavyotrendi na kushika nafasi ya kwanza na wimbo wake wa All Night aliomshirikisha msanii mpya aitwaye Angella ndivyo anavyomsababishia msala Mondi ambaye baadhi ya mashabiki wanadai kuwa hawapi kile wanachokitaka badala yake wanalazimika kusikiliza nyimbo za Harmo ambaye ndiye anazungumzwa zaidi.
“Kiukweli Simba (Mondi) unavyotutenda sisi fans (mashabiki) wako siyo sawa.
“Ametunyima umbeya, akaona haitoshi na nyimbo nazo hakuna. Tunaishia kuimba na kucheza nyimbo za huyu jamaa (Harmo). Haki unatuvua nguo mashabiki wako hasa sisi Team Wasafi.
“Hebu ona mashabiki wako tunavyotia aibu, haki ya nani hebu vunja ukimya, toa nyimbo moja ya hatari umalize kabisa utawala wa mitandao wa huyo jamaa (Harmo) kwa hizi wiki kadhaa.
“Unajua Simba amenyamaza sana, amepoa kama maji kwenye mtungi, siyo yule Simba ambaye alikuwa hakaukiwi na udambwidambwi wa Instagram, mara anatoka na pisi kali, mara ameachana na mzazi mwenzake, sasa hebu ona anatishwa hadi na kinyago alichokichonga mwenyewe.
“Haki mjue nasikiliza huu wimbo wa Harmonize halafu ninalia kimyakimya. Ninaimba huku ninaumia roho.
“Nimejikuta tu kwani sasa nitafanyaje? Chibu (Mondi) siku hizi kimya. Bora hata zamani alivyokuwa anatupa umbeya kama wote, lakini sasa hivi ni Konde Boy (Harmo) na Kajala tu.
“Tunasema hivi siyo kwa ubaya, lakini ni kwa sababu tunampenda Chibu na tunataka awe anatrendi kuliko mastaa wote.” Ilisomeka sehemu ya maoni lukuki juu ya ukimya wa Mondi.
Ugonjwa huo wa kutotoa wimbo mpya ni kama ule uliomuandama staa nwingine wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’.
Kabla ya kuachana na utaratibu wa kukaa kimya muda mrefu, mara kadhaa King Kiba alilalamikiwa kwa kushindwa kutoa nyimbo nyingi ambapo kwa mwaka mzima aliishia kuachia ngoma tatu pekee.
Hadi sasa, Mondi hajaachia ngoma mpya tangu mwaka huu umeanza zadi ya kushirikishwa na Baba Levo kwenye Wimbo wa Shusha na Lava Lava kupitia Nyimbo Bado Sana na Far Away.
Kwa upande wake, Harmo anasisitiza; “Huu ni mwaka wangu wa kuwa kileleni mwaka mzima bila kushuka kwenye trending za mitandao ya kijamii.”
Stori: Khadija Bakari, Dar