
KUELEKEA kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan, tayari imebainika kwamba, Simba wamezinasa siri za wapinzani wao hao mapema.Siri hizo zimevujishwa na mashushushu wao waliotangulizwa nchini Sudan kabla ya kikosi cha timu hiyo kufika huko tayari kwa mechi.
Taarifa kutoka ndani ya Simba, zinasema kwamba, wametakiwa kutosafiri kizembe na kutakiwa kwenda kwa tahadhari kubwa bila ya kusahau kubeba vyakula ili kujiweka salama zaidi kwani kuna hujuma zimeandaliwa Leo Jumanne, Simba wanatarajiwa kusafiri kuelekea Sudan kwa ajili ya mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi utakaochezwa Jumamosi ijayo.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, tayari Simba wameshawatuma wawakilishi wao nchini Sudani ili kujua hali ilivyo huko na mambo mengine muhimu kabla ya timu hiyo kuwasili.

“Mechi yetu na Al Merrikh ya Sudan haitakuwa nyepesi, maana jamaa wamepania sana na kwamba imefikia hatua ya mashabiki kwenda kumtishia rais wa timu yao wakimtaka abwage manyanga, jambo ambalo limemfanya kuahidi ushindi.
“Watu wetu waliotangulia kule wametutaka kuhakikisha tunajitahadharisha na suala la chakula na maji jambo ambalo linatufanya sasa tufikirie zaidi kusafiri na vyakula kwani mechi hiyo imeshaonekana kuwa na presha kubwa kwao,” kilisema chanzo hicho.
Tayari Simba imeshacheza mechi mbili za hatua hiyo dhidi ya AS Vita ya DR Congo na Al Ahly ya Misri ambapo zote imeibuka na ushindi na kuongoza Kundi A ikikusanya pointi sita.
Al Merrikh yenyewe ikiwa nayo imecheza mechi mbili, imepoteza zote.
STORI NA MUSA MATEJA | SPOTI XTRA