
WATU wasiokula mayai na kuku wamepewa tahadhari dhidi ya kupewa chanjo ya Corona kwani inaweza kuwadhuru kwa njia mbali mbali ingawaje shirika la Afya Duniani WHO halijatoa mwongozo kamili kuhusu hilo . Wizara ya Afya ya Kenya ndio iliyotoa ilani kwa watu wasiotumia mayai na kuku dhidi ya kuipokea chanjo hiyo.
‘Kuna utaratibu unaofaa kufuatwa kabla ya kupewa chanjo hiyo na iwapo unajua utapatwa na madhara ukidungwa chanjo yenye protini ya mayai au kuku basi hakikisha unaiepuka chanjo hii’ amesema katibu wa kudumu wa Wizara ya Afya Susan Mochache.
Hata hivyo kulingana na Kituo cha kudhibiti na kuzuia maradhi CDC ,watu wasiotumia mayai na kuku kama chakula wanaweza kupewa chanjo hiyo chini ya mazingira ya ‘kimatibabu’ ili kuweza kushughulikia madhara yoyote yanayoweza kutokea.

Je, chanjo hiyo inaweza kuwa na madhara yapi?
Uhusiano uliopo kati ya chanjo ya Corona na protini ama vyakula kama mayai na nyama ya kuku ni kwamba virusi hudungwa ndani ya protini hiyo ili kuzalishwa zaidi na baadaye kusafishwa lakini hilo haliondoi kabisa kiungo cha protini kutoka chanjo yenyewe na hivyo basi kumdhuru yeyote ambaye hafai kula mayai au nyama ya kuku.
Kulingana na mwongozo wa WHO , chanjo kwa watu walio chini ya umri a miaka 18 haipendekezwi. Pia kuna mjadala unaoendelea wa iwapo watu wengi watakubali kwa hiari kupewa chanjo hiyo kwani wengi hawafahamu inavyofanya kazi ni iwapo ina madhara ya pembeni hata kwa wasiokula nyama ya kuku na mayai.
Serikali ya Kenya inapanga kuwachanja takriban watu milioni moja kutumia awamu ya kwanza ya dozi zilizowasili nchini siku ya jumanne usiku .Awali kulikuwa na mpango wa kuwachanja watu 500,000 kutumia shehena hiyo ya kwanza ya chanjo na dozi ya pili wiki nane baadaye.
Hata hivyo wizara ya Afya imesema kuna mpango wa kupata shehena ya pili ya chanjo hiyo katika wiki tatu au nne zijazo pakiwa na hakikisho kwamba patakuwa na chanjo ya kutosha kuwadunga watu kwa awamu ya pili ya dozi hiyo iwapo itahitajika.
Shehena ya kwanza ya chanjo hiyo iliwasili Nairobi kutumia ndege ya Qatar Airways QR1341 na kupokelewa na maafisa wakuu wa serikali wakiongozwa na waziri wa Afya Mutahi Kagwe ,mwakilishi wa Unicef nchini Kenya Maniza Zaman na mwakilishi wa WHO nchini Kenya Dr Rudi Eggers.
Shehena ya kwanza ya dozi milioni 1.02 ni sehemu ya kifurushi cha mwanzo cha dozi milioni 3.56 zinazofaa kupewa Kenya.