×

Mifumo Ya Kocha Mpya Yanga Yavuja, Yambeba Carlinhos, Niyonzima

KAMA Yanga ikifanikiwa kumnasa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Township Rollers ya nchini Botswana, Nikola Kavazovic, basi itakuwa imeramba dume kutokana na mifumo miwili matata anayoitumia katika kupata ushindi.

 

Kavazonic ni kati ya makocha wanaotajwa kuja kuchukua mikoba ya Mrundi Cedric Kaze ndani ya kikosi cha Yanga mara baada ya kusitisha mkataba wa kocha huyo.

 

Yanga hivi karibuni ilifikia uamuzi wa kulivunja benchi lake la ufundi kutokana na timu yao kupata matokeo mabaya, hivi sasa ipo kwenye mchakato wa kumpata kocha mkuu mpya.Kocha huyo raia wa Serbia, mwenye leseni ya Uefa, ana mifumo miwili ya uchezaji ambayo ni 4-2-3-1, 4-2-1-3 yote ya kushambulia na kujilinda ndani ya 90 wakati mchezo unaendelea.

Mifumo hiyo itawabeba wachezaji viungo wachezeshaji na washambuliaji ambao ni Carlos Fernandez ‘Carlinhos’, Tuisila Kisinda, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mukoko Tonombe, Yacouba Songne na Said Ntibazonkiza ‘Saido’.

 

Kocha huyo akitumia mfumo wa 4-2-3-1 atatakiwa kucheza soka la pasi fupi za haraka na kupiga mipira mirefu ya kushtukiza kwa mshambuliaji mmoja atakayekuwa kwenye goli la wapinzani huku nyuma yake akiwa na viungo watatu watakaomchezesha.

Akitumia mipira mirefu, kocha huyo atatakiwa kumtumia Carlinhos kutokana na umahiri, uwezo wake mkubwa alionao katika upigaji wa mipira akitumia miguu yote miwili kufikisha pasi kwa washambuliaji.

Mserbia huyo akibadilisha mfumo na kutumia wa 4-2-1-3, atatakiwa kutumia washambuliaji watatu wenye uwezo mkubwa wa kufunga huku nyuma yao akiwemo mmoja mwenye uwezo wa kupiga pasi mpenyezo za mwisho nzuri zitakazofika kwa washambuliaji hao watatu ambaye na mwenye uwezo huo ni Niyonzima.

 

Washambuliaji hao watatu watakaocheza mbele ya Niyonzima ni Yacouba, Saido na Tuisila wachezaji wenye kasi na uwezo mkubwa wa kulishambulia goli la wapinzani huku wakifunga mabao.

 

Awali, Yanga iliyokuwa inafundishwa na Kaze yenyewe ilikuwa ikitumia mfumo wa 4-5-1 na 4-4-2, lakini Kavazovic yeye atakuja na mifumo ya kisasa itakayoshambulia, kupiga pasi fupifupi na kushambulia kwa kasi akiwatumia viungo wengi washambuliaji.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, Kavazovic alishapigiwa simu na viongozi wa Yanga ili kujua ofa yake na mambo yanaendelea vizuri huku pia Wanajangwani hao wakijaribu kuangalia CV za makocha wengine mbalimbali kabla ya kumpata mmoja atakayekuja kuungana na Juma Mwambusi atakayekuwa msaidizi.

Akizungumzia hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli alisema kuwa: “Bado mchakato wa kumpata kocha mkuu unaendelea katika timu na upo chini ya kamati ya utendaji.

 

“Jumla ya CV 72 tumezipokea kutoka kwa Mkocha mbalimbali kutoka Ulaya na Afrika, mara baada ya kuzipitia tutatafuta CV za makocha watatu na kati ya hayo atapatikana mmoja ambaye tutamtangaza.”

 

Kocha huyo aliwahi kuzifundisha timu za BASK (1996–2005), OFK Žarkovo (2006–2008), Borac (2008–2010), Resnik (2010–2012), FC Istiklol (2012–2013), Tajikistan (2012–2013), Sri Lanka (2014–2015), New Radiant (2015), Lanexang United (2016), New Radiant (2016), Saif (2016–2017), Township Rollers (2017–2018), AFC Leopards (2018), na Free State Stars (2018–2019).

STORI NA WILBERT MOLANDI

Leave a Comment