×

Mama Samia: Rais Magufuli Anawasalimia Sana – Video

 

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan amewatoa hofu Watanzania wote kutokana na hofu inayoenezwa mtandaoni kuwa Rais Dkt. John Magufuli yupo nje ya nchi anatibiwa.

 

Mama Samia amesema hayo leo Jumatatu, Machi 15, 2021 akiwa ziarani mkoani Tanga na kusisitiza mshikamano na kutosikiliza maneno ya watu kutoka nje ya Tanzania.

 

“Nimekuja hapa (Tanga) niwasalimie lakini kubwa niwape salamu za Rais, Rais anawasalimia na anawashukuru sana kwa kazi nzuri mliyofanya mwaka jana kurudisha Serikali ya CCM madarakani, Rais anasema tupo salama, tuchape kazi, twende vizuri,tujenge upendo na mshikamano.

 

 

“Nataka niwaambie kwamba, katika wakati muhimu wa Watanzania kushikamana ni huu, kujenga umoja ni wakati huu, si wakati wa kusikiliza maneno ya nje nasi yakatuparanganya vichwa. Niwaombe Watanzania wote tushikamane na tuchape kazi ili Taifa letu lisogee.

 

 

“Niwahakikishie Wananchi, Tanzania tuko salama, chapeni kazi ili kuleta maendeleo, uimara wa Taifa letu unaleta maneno mengi, msibabaishwe na maneno ya Watu walioko nje,” amesema Mama Samia.

 

 

Kauli hii ya Makamu wa Rais inakuja wakati kukiwa na uvumi katika mitandao ya kijamii kuhusu kutokuonekana hadharani kwa Rais John Magufuli tangu Jumamosi, Februari 27.

 

 

Siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alivunja ukimya na kueleza kuwa Rais Magufuli anaendelea na shughuli zake kama kawaida na si lazima aonekane kila siku.

 

 

Hadi sasa watu wanne wamekamatwa kwa tuhuma za kusambaza uvumi kwenye mitandao ya kijamii kuwa Rais Magufuli anaumwa.

 

 

Leave a Comment