
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amemweleza Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwa, aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli amefungua barabara ya maendeleo Tanzania ambayo anapaswa kuifuata.
Kenyatta amemtia moyo Rais Samia na kusema kuwa, licha ya kupokea uongozi katika kipindi kigumu cha majonzi, Mwenyezi Mungu ataendelea kuwa pamoja naye na kumsaidia, hivyo anapaswa kuwa na moyo mkuu.
Kenyatta ambaye kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) amesema kuwa, nchi zote za Ukanda wa Afrika Mashariki zipo pamoja na Tanzania kuomboleza msiba huo mkubwa wa Dkt Magufuli.
“Nipo hapa kumuombeleza rafiki wa karibu ni mtu ambaye tulikuwa tunaongea mara kwa mara, kwangu mimi ni pigo kwa sababu alikuwa ni mtu wa heshima na ndipo tukasema ya kwamba iwe liwalo lazima nije kuungana nanyi kumsindikiza ndugu yetu.
“Kwa muda wa miaka michache ameonesha ya kwamba sisi kama Waafrika tuko na uwezo wa kujitoa kuwa tegemezi kwa watu na nchi za nje na tupo na uwezo kama Waafrika kusimamia uchumi wetu na kuhakikisha ya kwamba wananchi wetu wanatendewa haki.
“Na sina shaka nikisema hapa leo ya kwamba Dada yangu Suluhu Samia na sasa Rais mwenzangu barabara umeoneshwa na ndugu yetu Dk Magufuli, Hapa ni kazi tu, wananchi wa Tanzania wapo nyuma yako endeleeni na umoja mliokuwa nao.
“Nikupe neno moja dada yangu Samia, umeshika nchi kipindu kichungu cha majonzi, hata Joshua alipoachwa na Musa alijiuliza nitaweza kweli, lakini Mungu alimwambia usiogope, kuwa na moyo mkuu, nawe usiogope mungu yu pamoja nawe,” amesema Kenyatta.
Amewataka Watanzania kuendeleza falsafa ya Dkt. Magufuli ya “Hapa Kazi Tu” ambayo imesaidia kuleta mabadiliko katika nchi ya Tanzania na kuhamasisha maendeleo katika eneo lote la Afrika Mashariki.