
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa , amesema Hayati Dkt. John Magufuli ameacha alama kubwa kwa watanzania, ameyasema hayo leo Machi 24, wakati akizungumza na maelfu ya waombolezaji na wananchi wa Mkoa na Jiji la Mwanza na mikoa jirani kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania.
Majaliwa alisema Rais Magufuli alikuwa kiongozi mahiri aliyeliongoza taifa hili kwa weledi mkubwa na kwamba vilio vya uchungu vya wananchi vinaakisi mazuri aliyoyafanya.
“Hatuna maneno marefu, ni tukio la muda mrefu tangu Machi 20, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaongoza wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kutoa heshima za mwisho,hii leo ni mwendelezo wa kuamuaga kiongozi wetu,”alisema Majaliwa.
Alisema Mkoa na Jiji la Mwanza ni eneo la kihistoria kwani Rais Magufuli, aliwahi kuishi na kufanya kazi wakati wa uhai wake na amejenga makazi yake.
Waziri Mkuu huyo alisema Hayati Rais Magufuli ameacha alama kubwa mkoani Mwanza na mikoa ya Kanda Ziwa kutokana na kazi alizofanya kwa kutekeleza miradi ya maendeleo lakini pia ameacha alama kwa taifa zima hadi vijiji.