
RAIS Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete amesema kuwa waliomsema kuwa hakukata jina la Dkt. John Magufuli kwenye kinyang’anyiro cha urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015 ni waganga njaa.
Mzee Kikwete amesema hayo leo katika uwanja wa Magufuli, Chato wakati akitoa salam za rambirambi kwenye ibada ya kumuaga na maziko ya hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa awamu ya tano wa Tanzania.
“Kila nilipopata fursa ya kutembelea hapa Chato nilipokuwa waziri na hata rais sikuacha kufika nyumbani hapa kumsalimia mama yetu (mama mzazi wa hayati Magufuli) nilikaa naye kwenye mkeka tukazungumza ya mama na mwanaye
“Mimi na mpendwa wetu John Magufuli, amekuwa Waziri wangu kwa miaka 10 nikiwa rais,kwa kuwa alikuwa mtani wangu yeye alikuwa ndio waziri pekee aliyeweza kunitania kila tulipokutana wengine walikuwa hawawezi, alikuwa jembe langu, ndio maana nilimuweka kwenye Wizara tatu zilizokuwa ngumu anyooshe mambo.
“Alipojitokeza kuomba uteuzi wa kuwa mgombea wa Urais wa CCM mwaka 2015, sikusita kumpendekeza katika majina matano niliyoyafikisha kwenye kikao cha juu cha chama, sikuwa na tabu na Magufuli ndio jina la kwanza halafu yakafuata mengine.
“Waswahili wanasema akutukane hakuchagulii tusi unaposikia minong’ono kwamba unasikia Kikwete hakumtaka Magufuli mimi labda Kikwete mwingine nimewasimulia leo mchakato tulivyokwenda na yale majina matano nilikuja nayo mimi tumepambana nayo mpaka yakatoka na la kwanza lilibaki kuwa la JPM nililoliweka mie nashukuru kwenda hadi mkutano mkuu ikawa hivyo hivyo.
“Oooh… Kikwete anamchukia Magufuli eeh labda mwingine si mimi namchukiaje mtu uliyemkabidhi ilani ya uchaguzi na ameitekeleza kwa kiwango cha juu sana lakini nikasema dunia waganga njaa wengi wanapata ulaji wao kwa kuongopa.
Tulitamani amalize kipindi chake cha uongozi na astaafu aone matokeo ya matunda ya kazi yake ila haikuwa hivyo, imetusikitisha sana ,” amesema Rais Kikwete.