
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema ombi lao la kukutana na Rais Samia Suluhu limekubaliwa na wakati wowote watakutana na kiongozi huyo.
Ombi hilo liliombwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyemuandikia barua Rais Samia mapema Aprili mwaka huu akiomba kuonana na uongozi wa chama hicho kwa ajili ya kumueleza masuala mbalimbali.
Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika ameyasema hayo leo Jumapili Aprili 25, 2021.
“Naomba kuwapa taarifa rasmi kuwa Aprili 20, 2012 tulipokea majibu ya barua ya Mwenyekiti Freeman Mbowe ya kuomba kukutana na Rais Samia. Rais amekubali kukutana na kushauriana na Chadema, tunasubiri kujulishwa tarehe ya kukutana.”
Hatua ya Rais Samia kukubali ombi la Chadema limekuja siku chache baada ya kuhutubia Bunge na kueleza kuwa anakusudia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa Tanzania ili kuweka mwelekeo wa kuendesha shughuli za siasa zenye tija na maslahi kwa nchi.
“Katika kulinda uhuru wa kidemokrasia nakusudia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa Tanzania ili kwa pamoja tuweke mwelekeo wa kuendesha shughuli za siasa zenye tija na maslahi kwa ajili ya nchi yetu,” alisema Rais Samia.