×

Masikini Nyumba za Yamoto, Miaka sita Baada Ya Kusabaratika

Nyumba ya Beka Flavour.

MASKINI! Unaambiwa mji haushiwi na mambo, ni bora mtu akunyime kula, lakini siyo ubuyu!

MASHTAKA MAZITO

Hivi karibuni ‘mahakama’ ya Gazeti la IJUMAA imepokea ‘mashtaka’ mazito juu ya nyumba zile walizojengewe wasanii wa iliyokuwa Yamoto Band.Madai yenyewe kutoka kwa vyanzo vya ndani yalidai kwamba, kuna mambo mawili; ama nyumba hizo zimetelekezwa na wenyewe au wamedhulumiwa.

 

Yamoto Band iliundwa na wasanii wakali wanne ambao ni Aslay Isihaka ‘Dogo Aslay ’, Mbwana Yusuf Kilungi ‘Maromboso’ ambaye kwa sasa anajulikana kama Mbosso, Beka Flavour na Enock Bella; shukrani ziende kwa Mkubwa Fela na lebo yake ya Mkubwa na Wanawe kabla ya kusambaratika mwaka 2015, yapata miaka sita iliyopita.

Aslay Isihaka ‘Dogo Aslay’

TUJIUNGE MBANDE-KISEWE

Mijengo hiyo ya aina yake ambayo ipo eneo la Mbande-Kisewe, Mbagala jijini Dar, ilianza kuonekana kupoteza mvuto, jambo lililosababisha baadhi ya

watu wakiwemo majirani kudhani kuwa huwenda wasanii hao wamedhulumiwa haki yao.

Nyumba ya Dogo Aslay.

TATIZO NI NINI?

Ilidaiwa kuwa baada tu ya Yamoto Band kusambaratika na kila mtu kuanza upya maisha yake mapya ndiyo sababu kubwa iliyosababisha wao kudhulumiwa mijengo hiyo ya kifahari.“Jamani hizi nyumba kiukweli zimepoteza kabisa mvuto; yaani siyo kama zilivyokuwa mwanzo, halafu tangu Fela atangaze kuwa ameamua kuwajengea wale watoto nyumba, mbona hatuwaoni wakiishi humo?

Mbwana Yusuf Kilungi ‘Maromboso’ ambaye kwa sasa anajulikana kama Mbosso.

“Yaani nyumba zipozipo tu, ni kama zimetelekezwa, kwa tulivyosikia ni kwamba alitaka awakabidhi nyumba zao kipindi bado wapo pamoja, sasa kile kitendo cha wao kugawanyika na kila mmoja kuanzisha maisha yake mapya ndiyo sababu kubwa iliyofanya mpaka sasa wasipewe nyumba zao, ninyi njooni mjionee wenyewe, hatujui kama wamedhulumiwa au la,” alisema mmoja wa majirani kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Enock Bella.

IJUMAA KAZINI

Baada ya kupata taarifa hizo, Gazeti la IJUMAA huwa halilazi damu hivyo liliingia kazini kwa kufunga safari hadi kwenye nyumba hizo na kufanikiwa kujionea ambavyo baadhi yake zimechakaa na kuonekana hazitumiki kabisa, lakini nyingine tayari zimekarabatiwa na kuna watu ambao wanaishi.

Nyumba ya Mbwana Yusuf Kilungi ‘Maromboso’.

MPANGAJI AZUNGUMZA

Gazeti la IJUMAA lilibisha hodi na kufunguliwa geti ambapo alitoka mama mmoja aliyejitambulisha kuwa yeye ni mpangaji wa mmoja wa mijengo hiyo na haya ndiyo yalikuwa mazungumzo yake na Gazeti la IJUMAA;IJUMAA: Habari yako mama?

 

MPANGAJI:

Salama, karibuni…IJUMAA: Asante, samahani tunawaulizia hawa wasanii (anatajiwa majina) wenye hizi nyumba sijui tumewakuta?

MPANGAJI: Mnamaanisha akina Mbosso?

IJUMAA: Eeh! Ndiyo haohao.

MPANGAJI: Kwa bahati mbaya hawapo, labda jaribuni kumtafuta mlinzi hapo nje, anaweza kuwasaidia.IJUMAA: Sawa, lakini tuliambiwa kuwa tukifika hapa tutakutana nao.

MPANGAJI: Hapa hawaishi, naishi mimi mpangaji.

 

IJUMAA: Ahaa! Kwa hiyo wameamua kupangisha nyumba zao?

MPANGAJI: Ndiyo, wamepangisha, mfano kama mimi hapa hii nyumba ninayoishi ni ya Mbosso na kila kodi inapoisha huwa anakuja kuchukua pesa yake.

 

IJUMAA: Mmmh! Mbona tuliambiwa kuwa hizi nyumba wamedhulumiwa?

MPANGAJI: Hapana, hizi nyumba hawajadhulumiwa, ila kuna utaratibu mdogo tu ambao ilitakiwa waufuate ndipo wakabidhiwe nyumba zao kama walivyofanya Mbosso na Beka Flavour.

 

IJUMAA: Ni utaratibu gani huo?

MPANGAJI: Unajua hizi nyumba zilijengwa, lakini finishing (ukamilishaji) ilikuwa bado kwa hiyo inatakiwa msanii mwenyewe amfuate Fela kisha ndiyo apewe hati yake ya nyumba, lakini waliofanya hivyo ni wawili tu; Mbosso na Beka, wao walimfuata Fela, akawapa hati zao, wakaja kwa viongozi wa Serikali ya Mtaa wakaandikishiana, basi mwisho wa siku wakapewa funguo zao na sasa nyumba ni za kwao, lakini Aslay na Enock ndiyo hawajafanya hivyo, kwa hiyo nyumba zao zipo tu zenyewe,” anasema mama huyo.

 

MBOSSO ANENA

Gazeti la IJUMAA lilizungumza na mmoja wa wasanii hao, Mbosso ambaye amethibitisha kuwa nyumba yake hiyo kwa sasa ipo tayari na ameshakabidhiwa kila kitu na Mkubwa Fela.“Nyumba ipo na Mkubwa ameshanikabidhi kila kitu,” anasema Mbosso.

UKWELI KUTOKA KWA BEKA

Kwa upande wake, Beka anaeleza ukweli kuhusu nyumba hizo;“Hakuna aliyedhulumiwa nyumba, hivyo ni vitu tu vinatengenezwa. Nyumba tangu zimeanza kujengwa zinaonekana na hadi waandishi wa habari waliitwa, sasa inakuwaje leo kuwe na mabadiliko kuhusu nyumba?

“Kila mtu ana nyumba yake pale na zimeshaisha bado vitu vidogo sana kukamilika na hapo kila mmoja anaweza kukamilisha mwenyewe na akiamua kuishi hapo sawa.“Mbosso ameshavuta na umeme kwake na amemuweka mtu anaishi pale ila sisi wengine bado hatujaweka watu.

 

“Narudia tena watu wafahamu Fela hahusiki tena na zile nyumba na mwanzo zinajengwa tulikubaliana sisi wahusika, pesa zitakazopatikana tusigawane, tumkabidhi Fela akatusimamie ujenzi kwa sababu sisi ilikuwa ni watu wa kusafiri sana, ikawa hatuwezi kupata pesa halafu tukasimamie ujenzi wakati hatupo Dar.“Lakini, tumeandikishiana na kila mmoja ameandika jina lake kwenye umiliki…

TUJIKUMBUSHE

Wakati Yamoto Band ikifanya kazi, Fela aliamua kuhakikisha kila msanii wa Yamoto anakuwa na mjengo.Akanunua viwanja na kuanzisha ujenzi huku akionesha makazi hayo kwenye vyombo vya habari. Wapo ambao hawakuamini, lakini baadaye kila kitu kikawekwa wazi.Lakini, baada ya kundi kuvunjika kila mmoja alisema lake kuhusu mijengo hiyo, lakini ukweli ndiyo huo.

STORI: MEMORISE RICHARD NA KHADIJA BAKARI, DAR

⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx

Leave a Comment