×

Ndugai Atoa Majibu “Mdee na Wenzako Chapeni Kazi” – Video

Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka wabunge 19 wa viti maalum ambao wamefukuzwa na chama chao cha CHADEMA kuendelea kuchapa kazi kwani wako katika mikono salama.

 

Ndugai ameeleza hayo leo Bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu, Mei 3, 2021 na kusema kuwa hawezi kuwaondoa bungeni Halima Mdee na wenzake 18 kwa barua tu, amesema katibu mkuu wa Chadema aandike barua, aambatanishe katiba yake na muhtasari wa hicho kikao kilichowafuta uanachama.

 

“Niwaambie vyama vya siasa, mimi ni Spika wa Bunge mzoefu, niko hapa bungeni kwa miaka 20 naelekea miaka 25. Nina uzoefu wa kutosha, wako watu wanapiga kelele kwamba Ndugai anavunja Katiba, hawajui walitendalo.

“Kwa katiba yao chama chao (wabunge 19), Baraza Kuu ndio chombo cha mwisho chenye maamuzi juu ya kufukuzwa kwao. Je, Baraza Kuu limekutana? Je, limefanya maamuzi ya mwisho? Watu wamekata rufaa Baraza kuu, wamesikilizwa? Sasa unawafukuzaje?

 

“Katibu Mkuu wa chama chochote unapoaniandikia barua juu ya jambo lolote lenye mgogoro, ambao unapelekea mambo ya kikatiba, usiniandikie kipeperushi tu, kwamba mimi fulani, fukuza fulani na fulani. Kazi yangu mojawapo ni kulinda wabunge.

 

“Nikipata Muhtasari wa kikao cha kuwafukuza (wabunge 19), nitaangalia je hawa wabunge wanaotuhumiwa kufukuzwa walipata nafasi ya kuhojiwa, kusikilizwa na kujieleza?, nifukuze watu ambao hawajasikilizwa kokote?

Ameeleza kuwa wengi wamekuwa wakilisifu Bunge la Tisa lililokuwa chini ya Spika Sitta lakini hawafahamu yeye alikuwa msaidizi wa karibu wa Spika Sitta akihudumu kama Mwenyekiti wa Bunge na ameshiriki kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza kanuni za Bunge zinazotumika sasa.

 

“Hivyo wabunge (wabunge 19) endeleeni kuchapa kazi, msiwe na wasi, mko mikono salama, na hiajapangwa Spika anaweza kuchukua hatua kwenye siku mbili au nne, ni busara yak tu, anakwenda taratibu, anajiridhisha. Kwanini watu wananiingilia?” amesema Ndugai.

Leave a Comment