×

Kenyatta: Ushirikiano wa Kenya na TZ Sasa Utakuwa wa Kiwango Kingine

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema ushirikiano baina ya Tanzania na Kenya utayafanya mataifa hayo kupiga hatua katika maendeleo.

 

Ameeleza hayo leo Jumatano Mei 5, 2021 katika kongamano la wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania lililofanyika mjini Nairobi, Kenya na kuhudhuriwa pia na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

 

“Tupo na nafasi na naamini kwamba tupo na nia ya kuhakikisha tukifanya pamoja tunaweza kuinua uchumi wa Tanzania na wa Kenya, naamini kwa dhati tukiingia kwa kazi hii kwa kushirikiana ushindi utakuwa wa wananchi wa nchi zetu mbili.”

 

“Tukijiona kama nchi zinazoshindana hatutaweza kupata wawekezaji wakubwa watakaowekeza kwenye viwanda kwenye nchi zetu na nchi za Afrika Mashariki…, vile ulitukumbusha jana Taifa la Kenya ni la tano kuwekeza katika Taifa la Tanzania tukiwa na kampuni 500, na tukasema kampuni za Tanzania ambazo zimewekeza nchini Kenya ni karibu 30,”amesema Kenyatta.

 

Katika ufafanuzi wake amebainisha kwamba, “Sisi tungependa kuona wawekezaji wengi zaidi Tanzania waje wafanye kazi zao hapa Kenya, nataka niseme leo kwamba wawekezaji wa Tanzania, mjue ya kwamba mko na uhuru wa kuleta na kufanya biashara zenu hapa bila kutishwa, mfanye kazi nchini Kenya kama mnavyofanya nchini Tanzania kwa kufuata sheria na kanuni ambazo zimewekwa.”

 

“Nina furaha tele na Wakenya wana furaha tele kwako Rais Samia Suluhu kukubali kuja kututembelea na Mimi sina shaka ya kwamba awamu yako ya uongozi wa Tanzania utaona uhusiano wetu kama majirani ukipanda kwa kiwango kingine cha juu juu juu zaidi,” amesema Kenyatta.

Leave a Comment