Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Mei 28, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (UN-Women) Dkt. Phumzile Mlambo-Ngcuka kuhusu kuendeleza agenda zinazowahusu wanawake Ikulu jijini Dar es Salaam.

Dkt. Phumzile amemshukuru Rais Samia kwa namna anavyounga mkono juhudi za kupigania masuala ya wanawake na ameahidi kuwa UN-Women itamuunga mkono katika juhudi hizo.

Amemualika kushiriki katika mkutano utakaojadilia masuala ya kijinsia uliopangwa kufanyika tarehe 30th Juni, 2021 huko Paris, Ufaransa ambao madhumuni yake ni kuchagiza usawa wa kijinsia kama yalivyokubaliwa katika mkutano wa Beijing uliofanyika mwaka 1995 baada ya kuonekana baadhi ya maazimio yanasuasua.
