The House of Favourite Newspapers

Nabi Aomba Michezo Mitatu Yanga

0

MARA baada ya kikosi chake kuingia kambini, Kocha Mkuu wa Yanga raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi ameomba michezo mitatu ya kirafiki kabla ya kurejea katika Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

 

Timu hiyo juzi ilianza mazoezi kwenye Uwanja wa Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa Juni 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Michezo ya ligi na Kombe la FA, hivi sasa imesimama ili kupisha kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars inayojiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi utakaopigwa Juni 5, mwaka huu.

Akizungumza na Championi Jumatano, Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema kuwa kocha huyo ameomba michezo hiyo kwa ajili ya kutengeneza fitinesi ya wachezaji wake.Saleh alisema kuwa, muda wowote huenda wakatangaza timu watakazocheza nazo mara baada ya kikao cha viongozi wa benchi kukutana na kujadiliana.

 

Aliongeza kuwa kati ya timu ambazo watakazocheza nazo ipo yao ya vijana U20 itakayochezwa kwenye Uwanja wa Avic Town na lengo kocha kupata nafasi ya kuiona timu ya vijana.

 

“Ngumu kwa timu kukaa wiki mbili bila kucheza mechi za kirafiki wakati tukiwa katika mashindano, hivyo wakati muda huu ligi imesimama kocha amependekeza tucheze michezo ya kirafiki.“

 

Lengo ni kutengeneza fitinesi na utimamu wa mwili ili ligi itakapoanza, basi wachezaji wake wawe tayari kwa ajili ya mapambano.“Zipo baadhi ya timu ambazo tutacheza nazo michezo ya kirafiki lakini kwa kuanza huenda tukacheza na timu yetu ya vijana ya U20 hapa kwenye Uwanja wa Avic Town,” alisema Saleh.

STORI: WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA

Leave A Reply