×

Mwanajeshi Ajiua Juu Ya Kaburi La Mkewe

ASKARI  wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Reginald Ruta amekutwa amekufa huku mwili wake ukiwa juu ya kaburi la mkewe, Godebertha aliyezikwa katika makaburi ya Mekyuri Kipawa jeshini mkoani Dar es Salaam.

 

Juni 7, mwaka huu mwili wa askari huyo aliyezikwa katika makaburi hayo jana, ulikutwa katika kaburi la mkewe aliyefariki dunia Alhamisi iliyopita baada ya kuugua ghafla.

 

Kifo cha askari huyo wa kambi ya Msata mkoani Pwani kimeacha simanzi kwa ndugu, jamaa na marafiki, kwa kuwa kilitokea siku tatu tangu mkewe afariki.

 

Akisoma risala kwenye ibada ya kuaga mwili wa askari huyo, iliyofanyika nyumbani kwake mtaa wa Karakata Kipawa, diwani wa Karakata, Idary Karugendo alisema marehemu ameacha watoto wanne na wajukuu watano waliokuwa wanamtegemea.

 

“Mzee Ruta alikuwa tegemeo kwenye familia yake kama baba, hasa baada ya kifo cha mke wake kutokea siku chache zilizopita,” alisema Karugendo.

 

Akizungumza katika ibada hiyo, Katekista wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Kipawa, Silivester Sadick alisema kifo hicho ni funzo kubwa kwa watu wote na kinaonyesha wazi hakuna binadamu mkubwa mbele ya Mungu.

 

Kwa mujibu wa jirani mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake, alidai kuwa walikuwa wote na Ruta siku ya Jumamosi ambayo yalifanyika mazishi ya mkewe aliyefariki ghafla wakati akijiandaa kwenda kazini.

Alisema baada ya mazishi Jumatatu iliyopita, vijana waliokuwa wanachunga mbuzi waliukuta mwili wake juu ya kaburi hilo.

Chanzo hicho kilieleza kwamba watoto hao baada ya kuona mwili huo wakaenda kutoa taarifa jeshini kwa sababu eneo hilo linamilikiwa na Jeshi na walipofika pale wakampekua hawakuona chochote zaidi ya kitambulisho chake.

Leave a Comment