
SERIKALI imewaelekeza wamiliki wa maeneo ya burudani na starehe kuzingatia matumizi ya vipima kelele na vizuia sauti kama inavyoelekezwa kwenye masharti ya leseni zao ili kulinda afya za wananchi kutokana na athari za kelele na mitetemo.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma Juni 29, 2021 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Seleman Jafo wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu udhibiti wa uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na vitu hivyo.
“Ili kuleta utulivu kwa jamii wamiliki wa nyumba za ibada, kumbi za starehe na burudani wahakikishe sauti zitokanazo na shughuli zao hazizidi viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Pia, amewataka wananchi kutoa taarifa kuhusu kero ya kelele na mitetemo katika ofisi za Serikali za mitaa au za NEMC kwa namba za bure 0800110115 au 0800110117.
Jafo amebainisha kuwa mwaka 2019/20, NEMC ilipokea malalamiko 165 katika Mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza, Morogoro na Tabora iliyohusu kelele kutoka nyumba za ibada, kumbi za starehe pamoja na baa.