
Taasisi ya matibabu ya CCBRT, leo imeishukuru Kampuni ya mawasiliano ya Tigo kwa kuendelea kuwachangia fedha za matibabu ya watoto wenye ulemavu wa miguu vifundo.
Akitoa msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari amesema kampuni yake inajisikia furaha kubwa ya kuendeleza ushirikiano wake na CCBRT katika juhudi za kuwasaidia watoto wanaozaliwa na ulemavu wa miguu vifundo.

“Leo tumechangia kiasi cha shilingi za Tsh. milioni 22 kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia watoto hawa ili wapone na kuondokana na ulemavu ili nao watimize ndoto za maisha yao wakiwa na afya njema. “Msaada wa pesa hizi unatarajia kusaidia kuwatibu na kuwaponya watoto zaidi ya 800. “Sisi kama Tigo tunajivunia mpango huu ambapo tangu tuanze kushirikiana na CCBRT miaka minne iliyopita tumeshawaponya watoto zaidi ya 4000,” alisema Mkurugenzi Karikari.

Akipokea msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT, Brenda Msangi amesema kwa niaba ya taasisi hiyo wanaishukuru sana Tigo kwa kuendelea kuwaunga mkono katika harakati za kumaliza tatizo la watoto wanaozaliwa na ulemavu wa miguu vifundo.

“Tigo wamekuwa wadau wetu kwa miaka minne sasa wakiendelea kutuunga mkono katika kuhakikisha watoto wanaozaliwa na tatizo hilo wanatibiwa na kuwa katika hali ya kawaida na kuepukana na ulemavu wa kudumu”.

“Tigo pamoja na kutusaidia pesa bali wanatusaidia namba ya kutuma ujumbe wa pamoja bure kwa wazazi wenye watoto wenye miguu vifundo kuja hapa CCBRT kuwapa matibabu bila malipo yeyote. “Hivyo naomba niwashukuru sana tena sana wadau wetu hawa na tunaomba wadau wengine wajitokeze kutuungana mkono katika kutokomeza tatizo hili maana tatizo ni kubwa sana kwasasa na linahitaji msaada zaidi wa kifedha,” alimaliza kusema Mkurugenzi Brenda.

Naye Daktari wa Mifupa ambaye ni mtaalamu wa kutibu tatizo la miguu vifundo, Prosper Alute amewaomba wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kwenye taasisi hiyo mapema mara tu waambiwapo na wataalamu wa afya kuwa wanatatizo hilo.

“Tatizo hili linapowahiwa mapema ni rahisi kupona lakini unapomchelewesha mtoto na kufikia miaka mitano mpaka kumi kunakuwa na ugumu katika matibabu”.
“Hivyo niwasisite tena wazazi na walezi kuwawahisha hapa watoto mapema wagunduapo tatizo hilo,” alimaliza kusema Dk. Alute. HABARI/PICHA ZOTE NA RICHARD BUKOS /GPL