×

Mastaa Wasiotaka Pesa Za Wanaume Wapo Hapa

Hakuna kitu kizuri duniani kama kuwa na vya kwako. Ninamaanisha uwe na kazi au biashara yako ambayo mwisho wa siku itakufanya kumiliki pesa zako mwenyewe na kuepuka kuwa tegemezi.

 

Kibongobongo wapo warembo wengi na wengine siku hizi hupenda kujiita pisi kali, huku wengine wakijiita slay queens, baadhi yao hupenda mno maisha ya mteremko.

 

Yaani kuvaa, kula na kulala kwao mara nyingi hutegemea pesa kutoka kwa wanaume bila kujishughulisha na hii ipo hata kwa baadhi ya mastaa Bongo ambao mara nyingi wamekuwa wakionekana kwenye kumbi za starehe na kutembelea magari ya kifahari huku kazi wanazofanya zikiwa hazijulikani.

Lakini kila penye baya na jema pia lazima liwepo. Leo, kupitia gazeti namba moja la mastaa ndani na nje ya Bongo la IJUMAA linakuletea listi ya baadhi ya mastaa wa kike Bongo ambao ukiwaangalia ni pisi balaa, lakini kichwani zimo na wanazisaka pesa ile mbaya;

 

WOLPER

Jina lake halisi ni Jacqueline Wolper Massawe. Unaweza kumuita Mama P. Ni staa kutoka katika kiwanda cha filamu Bongo. Amewahi kutamba na muvi kama Red Valentine, Family Tears, Dereva Taxi, Tom Boy na nyingine nyingi, lakini kwa sasa anatamba kwenye Tamthiliya ya Pazia.

 

Sifa ya kuwa ni binti wa kichaga ndiyo inayombeba kwani mwanamama huyu anapiga kazi ile mbaya. Amefanikiwa kufungua maduka kadhaa jijini Dar ambapo moja anauza vitenge na lingine anauza vitambaa na nguo za akina dada.

 

Ukitaka ugombane na staa huyu, basi wewe mzingue tu kwenye biashara zake. Ni mwanamke ambaye amekuwa akikaririwa akisema kwamba huwa halali. Anakesha akitafuta pesa na kweli  matunda ya biashara zake yanaonekana.

 

ESHA BUHETI

Huyu ni mwanamama mwingine wa chuma kutoka Bongo Movies. Esha amebarikiwa kipaji kikubwa cha kuigiza. Akiwa mbele ya kamera, hutachoka kumtazama.

 

Alianza kidogodogo na biashara yake ya mamantilie, lakini Mungu ni mwema kwani kwa sasa ni mamantilie mkubwa na wa kuaminika. Anapata oda za kupika chakula kwenye sherehe mbalimbali. Amefungua mgahawa wa kishua nyumbani kwake, Kijitonyama jijini Dar lakini pia hivi karibuni alitoka kuzindua tawi lake jipya jijini Dodoma.

 

SHILOLE

Jina alilopewa na wazazi wake ni Zuwena Mohammed ila wengi wanamfahamu kwa jina la Shilole au Shishi baby kutokana na kazi ya muziki anayofanya.

 

Ukiambiwa utaje listi ya mastaa wanaojua kutafuta pesa, basi naamini huwezi kuacha kutaja jina la mwanamama huyu. Ni mwanamke na nusu. Mbali na kazi yake ya sanaa ya muziki anayofanya, lakini pia ni mamantilie wa kishua anayemiliki Shishi Food maeneo ya Ada State, Kinondoni jijini Dar na Dodoma.

FAIZA ALLY

Huyu naye ni msanii wa filamu Bongo. Pia ni mama wa watoto wawili. Ni mwanamke mpambanaji hasa. Ukimfuatilia utaona jinsi anavyopambana na biashara zake.

Mara nyingi amekuwa ni mtu wa kusafiri nje ya nchi hasa China kwa ajili ya kuchukua mzigo kisha kuuleta Bongo.

 

HAMISA MOBETO

Ni mwanamitindo na msanii wa muziki wa Bongo Fleva. Mbali na urembo alionao, pia ni mwanamke ambaye anapambana ili kuhakikisha familia yake inaishi katika mazingira mazuri.

Mrembo huyu amefungua duka lake la nguo ambalo linapatikana maeneo ya Makumbusho jijini Dar na kuifanya biashara yake kutambulika zaidi ndani na nje ya nchi. Mbali na duka hilo la nguo za wakubwa, pia ana duka lingine la nguo za watoto ambalo lipo Mwananyamala jijini Dar.

 

MUNA LOVE

Jina lake halisi ni Rose Alphonce, ila wengi wanamtambua kwa jina la Muna Love kutokana na kazi ya sanaa ya uigizaji. Mwanamama huyu naye hajabaki nyuma kwani baada ya mtoto wake, Patrick kutangulia mbele ya haki miaka kadhaa iliyopita, alijiingiza rasmi kwenye biashara ya nguo za watoto inayojulikana kwa jina la Patrick Classic na kuvalisha watoto mbalimbali wa mastaa akiwemo Tiffah Dangote na Prince Nillan wa Diamond Platnumz na Zari.

Makala: Memorise Richard

Leave a Comment