
UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa unaunga mkono jitihada zote za uwekezaji zinazofanywa na mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ huku wakimuaga aliyekuwa msemaji wa timu hiyo, Haji Manara.
Mashabiki hao wa Simba waliungana ambapo jana Alhamisi katika Kijiji cha Makumbusho walitoa kauli zao juu ya kile kinachoendelea kwa sasa ndani ya klabu hiyo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Kiongozi wa Tawi la Wekundu wa Terminal, Justine Mgaigwa, alisema kuwa mashabiki wa timu hiyo wanatakiwa kutulia na kuacha kushabikia mambo ambayo yanaibomoa timu hiyo kwani wanatakiwa kuunga mkono jitihada za Mohamed Dewji ambazo zimeipa mafanikio makubwa klabu hiyo.

“Mashabiki wa Simba tunatakiwa kutulia katika kipindi hiki ambacho kuna mambo ambayo si ya msingi yanajitokeza, tunatakiwa kumuunga mkono Mo Dewji ambaye kiukweli ametutoa mbali sana Wanasimba na sio sisi kuvurugana hivyo tunachotakiwa kwa sasa ni kuelekeza nguvu zetu zote katika masuala ya msingi kama mabadiliko na kuelekea katika kilele cha Simba Day.“
Kuhusu Manara sisi Wanasimba tunamtakia kila lakheri uko aendako baada ya mambo ambayo aliyazungumza jana, hivyo tusingependa kuongea mambo mengine kwa kuwa Simba ni bora kuliko mtu yeyote yule.”
STORI: NA WAANDISHI WETU, Dar es Salaam