
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kifo cha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa kimeacha pengo kubwa sio tu kwenye familia, lakini pia kwenye serikali.
Amesema hayo Agosti 6, 2021 wakati wa kuaga mwili wa marehemu Kwandikwa katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam; “Hadi mauti yanamkuta Marehemu kama mnavyoelewa alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, hivyo ni wazi kifo chake ni pigo kwa serikali.
“Naelewa machungu mliyonayo wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia msiba huu mkubwa, naungana nanyi katika kipindi hiki cha majonzi na masikitiko, machungu yenu ndiyo machungu yetu namuomba Mungu akupeni faraja na moyo wa uvumilivu
“Kifo cha Mh.Kwandikwa kimeacha pengo kwa familia na serikali, hadi mauti yanamkuta alikuwa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, hivyo ni wazi kifo chake ni pigo kwa serikali,” amesema Rais Samia.
Aidha, Samia amesema wakati akiwa Makamu wa Rais, Marehemu Kwandikwa akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi wakati huo, alishiriki naye katika ziara iliyofanyika katika mikoa mitatu, Singida, Tabora na Shinyanga akionesha kuwa mtu makini, mfuatiliaji, mtulivu , msikivu na asiye na makuu.
Ameongeza kuwa Marehemu Kwandikwa alishiriki naye katika ziara hiyo na kuwa hakutoa sababu ya kutoka nje ya ziara hadi ziara inamalizika.