
IMEFAHAMIKA kuwa, kiungo mchezeshaji raia wa Mali, Sadio Kanoute, juzi jioni alijiunga na kambi ya Simba nchini Morocco kujiandaa na msimu mpya wa 2021/22.
Kiungo huyo aliyeletwa kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Mzambia, Clatous Chama, anasajiliwa na Simba kwa dau la dola 150,000 (zaidi ya Sh 348Mil) akitokea Al ahly Benghazi ya nchini Libya.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kiungo huyo tayari amejiunga na timu hiyo iliyopo Morocco na jana Jumatatu alitarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili.Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, mara baada ya kusaini mkataba huo, haraka atatambulishwa.
Aliongeza kuwa, kiungo huyo alipokewa na mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally kwenye Uwanja wa Ndege wa Morocco.
“Kanoute muda wowote atatambulishwa baada ya juzi (Jumapili) jioni kutua Morocco na kupokewa na uongozi wa Simba.“
Atatambulishwa baada ya kukamilisha taratibu zote za kitimu ikiwemo kusaini mkataba wa miaka miwili.“Baada ya kusaini leo (jana) ataanza mazoezi haraka pamoja na wenzake katika kujiandaa na msimu mpya,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Abbas kuthibitisha hilo, simu yake ya mkononi iliita bila ya mafanikio ya kupokelewa.
STORI: WILBERT MOLANDI, Dar