
KAMA ulikuwa unaamini vita kati ya mastaa wawili wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ na Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’, imekwisha basi unajidanganya kwani kimeumana upya, IJUMAA linakupa ubuyu wa motomoto.
Achana na lile sakata lao juu ya mtoto wa mwigizaji Kajala Masanja, Paula Paul, sasa vita nzito imeubukia huku, kila mmoja anataka kuonekana ni mkali na yupo juu kuliko mwenzake.
Iko hivi; wasanii wengi na wakubwa kwa sasa wanaachia nyimbo zenye ladha ya nchini Afrika Kusini; yaani Amapiano na huko ndiko vita mpya ya Harmonize na Rayvanny ilikoibukia.

Tangu wiki iliyopita, Harmonize alikimbiza na Wimbo wa Mang’dakiwe Remix akiwa ameshirikishwa na wasanii DJ Obza na Leone Lee kutoka Afrika Kusini, lakini Kibongobongo Konde Boy ndiye anaonekana kuwa kinara wa ‘songi’ hilo.
Wakati Harmonize akishikilia namba moja kwa siku kadhaa huku akijipa jina la Teacher (Mwalimu) wa Amapiano, ghafla Rayvanny ameibuka na Wimbo wa Chawa akiwa na Whozu na Ntosh Gazi kisha kutishia kumaliza ufalme wa Harmonize kwenye namba moja huku akijiita Lecturer (Mwalimu wa Chuo) cha Amapiano.
Tafsiri ni rahisi tu kwamba, anayejiita Mwalimu wa Chuo ambaye ni Rayvanny anafikisha ujumbe kwamba ni mkubwa kuliko Mwalimu wa Msingi au Sekondari ambaye ni Harmonize.Kufuatia hali hiyo, jana, Rayvanny aliposti ‘screen-shot’ iliyoonesha wimbo wake huo unashika namba moja ukihusisha na video za matukio na habari ikionesha anashika namba moja kisha akaandika; “Lecturer number unooo fukuzaaa chawaaa…
”Kwa mujibu wa mashabiki wa Rayvanny, ujumbe huo ni kijembe kwa Harmonize ambaye amekuwa akijiita Teacher hivyo vita imeibuka tena upya kwa mashabiki wa wawili hao kuendelea kurushiana vijembe.
Tangu kuondoka kwa Harmonize kutoka kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) chini ya Diamond Platnumz, uhusiano wa jamaa huyo na Rayvanny ambaye haujawahi kukaa sawa; kunachotokea ni kutulia kwa upepo tu kisha hali inakuwa ni ileile ya kupimana ubavu wa nani ni mkubwa kuliko mwenzake.
Stori: KHADIJA BAKARI, DAR