Rais John Magufuli akifanya usafi.
Na Mwandishi Wetu
Baadhi ya vijana wanaodaiwa ni watumiaji wa madawa ya kulevya ‘Mateja’ wenye maskani yao katika eneo la Feri jijini Dar, Jumatano iliyopita walikuwa miongoni mwa wananchi waliojitokeza kufanya usafi katika eneo hilo, wakiungana na Rais John Magufuli aliyeongoza shughuli hiyo.
Wananchi kote Tanzania waliungana kuadhimisha siku ya Uhuru wa Tanganyika kwa kufanya usafi maeneo mbalimbali nchini, wakitii maelekezo ya Rais Magufuli kuwataka kufanya hivyo ili kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza, hasa kipindupindu badala ya kuitumia siku hiyo kwa maandamano na hotuba.

….Akizoa taka.
Rais Magufuli alitoka nje ya eneo la Ikulu lililopo Magogoni na kuelekea Feri ambako shughuli za uvuvi na uuzaji samaki hufanyika, licha ya kuwahamasisha kufanya usafi pia aliwapa nafasi ya kueleza matatizo yao ambayo aliahidi kuyashughulikia kwa kile alichosema ni jirani yao.
Lakini baadhi ya vijana wanaotumia madawa ya kulevya pembeni mwa Bahari ya Hindi eneo hilo la Feri waliposikia kuwa mkuu wa nchi yuko eneo lao, waliacha mambo yao na kuungana naye katika suala la usafi.
Vijana hao walionesha kuvutiwa na maelezo ya rais hivyo kujitokeza kwa nguvu kubwa kuzoa takataka mara tu kiongozi huyo wa awamu ya tano alipowataka kufanya hivyo.
Wakitumia mikono, baadhi ya vijana hao wakiungana na raia wema walizoa taka na kuziweka katika matenga kisha kuzitupia katika gari la kusomba takataka lililokuwa limeegeshwa eneo hilo, kazi ambayo ilifanyika kwa dakika chache kabla ya Rais Magufuli kuondoka kurejea Ikulu akiwa pamoja na mkewe mama Janeth Magufuli na watendaji wengine wa serikali.
Big up our President…!!! Wishing you all the best