×

Polisi Wawadaka Watuhumiwa wa Ugaidi Wakiwa wa Silaha

Jeshi la Polisi nchini Kenya, limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wa ugaidi katika Kivuko cha Likoni, wakiwa njiani kuelekea jijini Mombasa.

 

Katika tukio hilo lililovuta hisia za wengi, polisi walilazimika kufyatua risasi hewani, kuwadhibiti wanaume hao waliokuwa ndani ya gari dogo, Toyota Probox lenye namba za usajili KCE 695U ambapo baada ya kufanikiwa kuwakamata, ndipo walipobaini silaha hizo zilizokuwa ndani ya gari hilo.

 

Silaha zilizokamatwa, ni bunduki mbili za kivita, AK-47, ‘magazine’ zilizokuwa zimejaa risasi, mapanga na mabomu yaliyokuwa yametengenezwa kienyeji.

 

Afisa Mkuu wa Polisi wa eneo hilo, John Elungata amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa polisi walifanikiwa kuwanasa wahalifu hao, Jumatatu ya Agosti 23, mita chache kabla hawajapita katika Kivuko cha Likoni.

 

Kwa mujibu wa chanzo kimoja, kukamatwa kwa wahalifu hao, kunatokana na taarifa za kiintelijensia zilizowafikia polisi baada ya kumkamata mmoja kati ya watuhumiwa hao, ambaye aliwaeleza kwamba wenzake wapo kwenye mpango wa kutekeleza shambulio la kigaidi katika Jiji la Mombasa.

 

Inazidi kuelezwa kuwa taarifa hizo ndizo zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa hao, ambao inaelezwa kwamba walikuwa wakitoka katika eneo la Lungalunga, wakiwa njiani kuelekea Mombasa.

 

Akaongeza kwamba wamefanikiwa pia kuzikamata simu za watuhumiwa hao na kwamba watu wote waliokuwa wakihusika kwenye mipango hiyo ya ugaidi, watatiwa mbaroni.

 

Tukio hilo limekuja muda mfupi baada ya Ubalozi wa Marekani nchini Kenya, kutoa tahadhari kwa raia wake kwamba kuna uwezekano wa kutokea kwa shambulio la kigaidi nchini humo.

Leave a Comment