×

Fredrick Mwakalebela Amfagilia Mayele

MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga, Fedrick Mwakalebela, ameibuka na kusema kuwa, hadi sasa tayari ana uhakika wa usajili uliyofanywa na timu hiyo, huku akisifia uwezo wa washambuliaji mpya raia wa DR Congo, Fiston Mayele.

 

Agosti 27, mwaka huu, kikosi chote cha Yanga kilichokuwa kimesalia nchini Morocco, kiliwasili tayari kwa kuungana na wenzao, kwenye tamasha la Siku ya Mwananchi, lililofanyika jana katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

 

Wachezaji hao ni pamoja na Djuma Shaban, Fiston Mayele, Yusuph Athan Tonombe Mukoko, Yacoub Sogne, Adeyun Saleh. Dickson Ambundo, David Nrayson na Abdalah Shaibu ‘Ninja’.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwakalebela amebainisha kuwa, kati ya wachezaji wote aliowaona wakati akiwa Morocco ni dhahiri kuwa tatizo la ubutu wa ufungaji ndani ya klabu hiyo linaenda kumalizika.

 

“Naomba niwahakikishie tu mashabiki wetu kuwa, Yanga hii tayari imeshaonyesha wazi kutatua tatizo la ubutu wa ushambuliaji, hasa kwa siku ambazo nimeona muunganiko wa Mayele na Yacoub Sogne wakifanya mazoezi Morocco.

 

“Naomba mashabiki wasubirie kuona uwezo mkubwa wa washambuliaji wetu mara tu baada ya michuano kadhaa kuanza,” alisema Mwakalebela ambaye alikuwa mkuu wa msafara huo.

 

MUSA MATEJA, Dar es Salaam

Leave a Comment