×

Mkuki moyoni mwangu – 07

WATOTO wawili (Kevin na Catarina) wapo katika mapenzi mazito lakini hakuna hata mmoja aliyefungua mdomo kumweleza mwenzake hisia zake, Kevin pamoja na kuwa mwanaume ana aibu nyingi, Catarina naye kwa upande wake anaamini mvulana ndiye anatakiwa awe wa kwanza kusema.

Kila siku wanazungumza wakiamini wao ni marafiki, lakini wote wanasubiri nani aanze! Mwisho wazazi wa Catarina wakaamua kumhamishia Kampala kimasomo walipogundua mtoto wao ameanza kuathiriwa na mapenzi katika umri mdogo.

Akiwa huko, Catarina anamkumbuka sana Kevin kiasi cha kuteseka, shule imefungwa na sasa amerejea Dar es Salaam, cha kwanza anachokitaka ni kumwona Kevin. Siku iliyofuata baada ya wazazi wake kuondoka kwenda kazini, aliamua kwenda Shule ya Sekondari ya St. Joseph kwa lengo la kumwona Kevin, akazuiliwa.

Badala ya kurejea nyumbani, aliamua kusubiri muda wa wanafunzi kutoka, akamwona Kevin ndani ya basi la shule na kumwita, hapo ndipo likatokea jambo ambalo hata yeye hakulitarajia; Kevin aliruka kupitia dirishani na kupiga kichwa kwenye barabara ya lami, damu zikaanza kumtoka puani, masikioni na mdomoni!

Catarina akakimbia mpaka eneo hilo na kumkumbatia, baadaye akaondolewa na Kevin akapakiwa kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Catarina akikodisha teksi. Hospitalini, hali yake inagundulika kuwa ni mbaya na anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kichwa kuondoa damu iliyovujia kwenye ubongo.

Wakati huo Catarina aliyekuwa amejificha kwenye kona moja hospitalini hapo, anajitokeza mbele ya wazazi wa Kevin ili kumjulia hali, anaishia kuambulia maneno makali kutoka kwa baba yake Kevin aliyedai kwamba yeye (Catarina), ndiye aliyesababisha yote hayo. Je, Kevin atapona? Nini zaidi kitaendelea?

ILIKUWA ni kumbukumbu mbaya maishani mwake, kwamba aliwahi kusababisha ajali ya mtu aliyempenda, Catarina kwa mara ya kwanza alijilaumu moyoni mwake ni kwa nini alikwenda shuleni kwa Kevin, asingekwenda Kevin asingeruka kutoka ndani ya gari lililokuwa likitembea kwa kasi na kupiga chini jambo lililosababisha awe mahututi na alikuwa katika hatari ya kupoteza uhai.

Machozi yalikuwa yakimbubujika akiyawaza hayo huku akitembea kuelekea kituo cha basi, alichotaka wakati huo ni kufika nyumbani kwao na kujifungia chumbani ambako angemlilia na kumwombea Kevin wakati wote upasuaji ukiendelea, sehemu fulani moyoni mwake alikuwa na tumaini kwamba asingekufa bali angetoka chumba cha upasuaji akiwa mzima mwenye afya njema na kurejewa na fahamu zake.

“Funga mdomo wako na ninakuomba uondoke mbele ya macho yangu sasa hivi, kabla sijakupiga…” ilikuwa ni sauti ya baba yake Kevin ikijirudia akilini mwake, tangu amfahamu mzee huyo, hata siku moja hakuwahi kumwona akiwa katika hali hiyo.

“Atanisamehe, sikufanya makusudi, yote ni sababu ya penzi nililonalo kwa mwanaye!” aliwaza Catarina.

Tayari alishafika kwenye kituo cha mabasi ya Muhimbili, akasonga mbele na kukifikia kituo cha teksi na kuchagua mojawapo ambayo aliingia na kuketi kiti cha nyuma, dereva aliyekuwemo ndani alimwangalia na kugundua alikuwa akibubujikwa na machozi.
“Pole sana, umefiwa?”

“Naomba unipeleke Masaki eneo la Kijiji NHC Estate!”
“Shilingi elfu tano.”
“Twende.”

Gari liliondolewa kwa kasi, hakuna aliyeongea chochote kati yao, Catarina aliendelea kububujikwa na machozi, mikononi mwake akiwa amebeba begi la Kevin ambalo ndani yake lilikuwa na madaftari pamoja na vitabu. Dakika ishirini baadaye alitoa sauti moja; “hapo mbele simama” dereva akakanyaga breki na kusimama mbele ya majengo ya Kijiji NHC Estate, Catarina akalipa shilingi elfu tano na kushuka.

Akapita lango kuu na kunyoosha hadi kwenye nyumba yao na kuingia ndani, hakuongea na mfanyakazi yeyote juu ya kilichokuwa kimetokea, badala yake alipandisha ngazi hadi chumbani kwake, akajifungia na kuanza kulia kwa uchungu akiliita jina la Kevin katika maombi yake kwa Mungu, ili amsaidie katika upasuaji uliokuwa ukiendelea chumba cha upasuaji Muhimbili.

Baadaye aliamua kufungua begi la Kevin na kutoa vilivyokuwemo ndani, macho yake yakatua juu ya daftari nene, fupi ambalo juu yake liliandikwa ‘My Journal’ moyo wake ukashtuka maana yeye pia alikuwa na daftari la aina hiyo ambamo aliandika kumbukumbu za mambo yote yaliyomtokea kwa siku, tangu alipoanza kujitambua.

Haraka akatupa madaftari pamoja na begi pembeni na kubaki na daftari hilo peke yake mkononi, haraka akaanza kuzifunua kurasa zake akitaka kufahamu ni kitu gani ambacho Kevin alikuwa akiandika kwenye daftari lake hilo la kumbukumbu, alielewa kilichoandikwa humo ndicho kingeeleza kila ambacho Kevin alikuwa nacho moyoni mwake na alichokuwa akifikiria kuhusu maisha:

Agosti 16, 1988, Academic International school
Tumehamia kutoka Tanga, baba amepewa uhamisho kuja jijini Dar es Salaam, amepandishwa cheo, hivi sasa ni Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanesco. Nimeandikishwa darasa la pili Academic International School ambako leo nimekutana na msichana mrembo sijawahi kuona! Kweli mimi ni mtoto mdogo, sitakiwi kujihusisha na masuala ya mapenzi, lakini msichana huyu ambaye jina lake anaitwa Catarina, amenivutia sana.

Nilimweleza baba tukiwa ndani ya gari juu ya uzuri wa msichana huyu, duh! Badala ya kufurahi mzee kawaaaka, yeye anafikiria mimi napenda ngono, ngono? Mimi mwenyewe sihitaji, nataka kupiga kitabu kwanza, mambo ya ngono baadaye, ila kiukweli, mtoto kanitia uchizi, ipo siku nitakuja kumwambia!

Agosti 17, 1988, nyumbani kwenye veranda
Oooops! Nimeongea na huyu mtoto leo, sauti yake laiiniii! Ya kumtoa nyoka pangoni, yeye mwenyewe nikimwangalia naona kama hajavutiwa na mimi kabisa, anaonekana mgumu, nilitamani nimweleze nampenda lakini nikasita, najifanya rafiki kwanza asinione nina haraka, isitoshe sisi wote bado watoto, nitakuja kumweleza baadaye, wasiwasi wangu kama wazazi wake wakihamishwa kwenda mkoa mwingine nitakuwa nimechemka!

Barua zilikuwa nyingi mno, zilizoelezea hisia ambazo Kevin alikuwa nazo kwa Catarina lakini alishindwa kuweka mambo wazi, Catarina aliendelea kuzisoma zote huku machozi yakimbubujika, hakuwahi kufahamu kwamba Kevin alimpenda kiasi hicho, akafumba macho na kuanza kumwomba Mungu ili amnusuru na kifo kilichokuwa kikimnyemelea chumba cha upasuaji.

Septemba 28, 1988,
nimeshindwa tena leo
Leo nilikuwa nimepania kabisa kumwambia Catarina ukweli wa moyo wangu lakini nilipokutana naye kwenye veranda nikashindwa kufungua mdomo, ulimi ukanasa kwenye sakafu ya mdomo, nampenda sana msichana huyu lakini naogopa kumweleza, pengine anaweza kukasirika halafu nikampoteza! Mungu nisaidie siku moja niwe na ujasiri wa kumweleza Catarina ninavyojisikia.

Barua nyingi ziliendelea lakini iliyomuumiza zaidi Catarina ni ile ambayo Kevin aliiandika siku ambayo yeye alikwenda shuleni St. Joseph na baadaye ajali kutokea, aliisoma machozi yakizidi kumbubujika na hakuweza kuimaliza hadi mwisho.

Juni 21, 1993, nimeota ndoto
Leo nimeota Catarina amerejea kutoka Uganda masomoni, ana furaha sana ya kuniona, kwa mara ya kwanza tumekumbatiana naye na kumpiga mabusu na nimemweleza kwamba ninampenda na amekubali kuwa mke wangu mara tukimaliza masomo ya chuo kikuu, amekuwa mrembo sana kuliko ilivyokuwa siku za nyuma, nampenda Catarina na sijui kama naweza kumwondoa akilini mwangu, juhudi zote za wazazi kunitenganisha naye kwa kumpeleka Uganda hakika zimeshindwa kuzaa matunda, Catarina ndiye mke wangu iwe isiwe!

Catarina alitupa daftari pembeni na kuanza kulia kwa uchungu mwingi, haukupita muda mrefu mlango wa chumba chake ukagongwa, aliponyanyuka na kuufungua alikutana ana kwa ana na wazazi wake, ndiyo walikuwa wamewasili kutoka kazini.
“Vipi Catarina mbona unalia?” baba yake aliuliza.

“Kevin amepatwa na ajali mbaya.”
“Ajali mbaya? Umejuaje?”
“Nilikwenda shuleni kwao.”
“Amepata ajali gani?”

“Aliponiona aliruka kutoka kwenye gari la shule likiwa kwenye mwendo kasi na kuanguka, akapiga kichwa kwenye lami, hali yake ni mbaya, yuko Muhimbili!”
“Mungu wangu! Wee mtoto! Unaona sasa?” mama yake Catarina alisema akionyesha masikitiko.Je, nini kitaendelea? Upasuaji unaofanyika Muhimbili utaokoa maisha ya Kevin? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.

Leave a Comment