
BAADA ya sintofahamu kuhusu usajili wa kiungo Khalid Aucho, uongozi wa Yanga umesema kuwa ushakamilisha kila kitu juu ya kiungo huyo na utamtumia katika michezo yote ya ligi kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Awali kiungo huyo ambaye yupo kwao akiitumikia timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ ilielezwa asingeweza kucheza michuano ya kimataifa kutokana na kibali chake cha uhamisho wa kimataifa (ITC) kushindwa kutolewa na timu yake ya El Macasa ya Misri.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederic Mwakalebela alisema kuwa tayari klabu hiyo ishakamilisha masuala yote ya yanayohusu vibali vya kazi vya mchezaji huyo hivyo atatumika katika michuano yote ambayo Yanga itashiriki mwanzoni mwa msimu.“
Aucho ni mali halali ya Yanga, tayari kama timu tulishakamilisha kila kitu ambacho kinahusu vibali vyake vya kufanyia kazi ndani ya Yanga na nchini, hivyo atatumika katika michezo yote ambayo Yanga itashiriki mwanzoni mwa msimu ujao ikiwemo Ligi Kuu, FA, Ngao ya Jamii na Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Aucho tulikuwa naye kule Morocco na kilichomuondoa kule ni majukumu ya kimataifa ya taifa lake la Uganda ambalo linashiriki michuano ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia na akimaliza majukumu yake basi atarejea nchini kujiunga na Yanga tayari kwa majukumu,” alisema kiongozi huyo.
LEEN ESSAU, Dar es Salaam