
JAMBO ambalo limewaacha midomo wazi Watanzania ni kuhusu mwanadada Mange Kimambi, Mtanzania aishiye nchini Marekani baada ya kukutana uso kwa uso na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye amekwenda nchini humo kwa ajili ya mkutano wa 76 wa Umoja wa Mataifa.
Ukiachana na masuala ya siasa, Mange pia amekuwa mdau mkubwa wa tasnia ya burudani na amekuwa akiwakosoa hadharani baadhi ya wasanii wakubwa akiwemo Diamond kwa mambo wanayofanya.
Mange ndiye aliyeratibu maandamano ya Aprili 26, 2018 kwa Watanzania walioko nchini na ambao wapo nje ya nchi licha ya maandamano hayo kushindikana kufanyika kutokana na kutopata sapoti ya kutosha.
Ikumbukwe kuwa, Mange amewahi kuingia kwenye malumbano na Serikali ya Tanzania hasa ile iliyokuwa chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wakati makamu wake akiwa Samia Suluhu, kupitia mitandao ya kijamii, Mange alikuwa akiwasema vibaya baadhi ya viongozi wakubwa akiwemo Rais bila woga.
Itakumbukwa pia wakati akimchachafywa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda, viongozi wengine wakubwa, wasanii na wakati mwingine watu wa kawaida mpaka ikafika wakati akakiri kwa mdomo wake kwamba hatorejea Tanzania labda maiti yake.
Hali hiyo ilimfanya kuonekana adui wa Serikali lakini cha kushangaza video zinazotrend mitandao kwa sasa ni dada huyo kuonana live na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Suluhu Hassan huku mama akitabasamu na kumwambia Mange “nimefurahi kukuona…”
Hii inatoa taswira gani za siasa za Mama Samia Suluhu Hassan na Tanzania kwa ujumla?