

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes Da Rosa, amevutiwa na uwezo wa beki wake mpya wa kati raia wa DR Congo, Henoc Inonga Baka, jambo linaloweza kumfanya afanye mabadiliko kwenye safu ya beki ya kati kwa kumuondoa Serge Pascal Wawa raia wa Ivory Coast kikosi cha kwanza.
Msimu uliopita katika safu ya ulinzi ya Simba, Gomes alikuwa akimtumia Pascal Wawa na Mkenya Joash Onyango, jambo ambalo kwa msimu huu linaonekana kubadilika kwa lazima baada ya kufanya usajili mpya wa beki kutoka DC Motema Pembe ya DR Congo, Henoc Baka, usajili ambao tayari umejibu kiasi cha kuamua kutengeneza muunganiko baina yake na Onyango.
Chanzo chetu kutoka kambi ya Simba iliyopo Karatu jijini Arusha, kimeweka wazi kwamba, takriban mazoezi yote ya kujiandaa kwa ajili ya msimu ujao, Gomes amekuwa akimpanga mara nyingi Baka kucheza na Onyango, katika eneo hilo la ulinzi wa kati.
“Naomba nikupe habari ambayo wengi hawajaitambua juu ya maandalizi yetu, ambayo ni kwamba tangu alipotua beki wetu wa kati Mcongo, Baka tayari mambo yamebadilika kabisa ambapo kocha Gomes amekuwa akimtumia kwenye ulinzi sambamba na Onyango jambo ambalo linaashiria Wawa anaweza kutokea benchi msimu ujao.
“Katika mechi zote za kirafiki ambazo tumecheza hadi sasa ni mchezo mmoja tu ambao Gomes hakumpanga Baka pamoja na Onyango, lakini mingine yote ukianzia tulipokuwa Morocco yote amekuwa akimpanga jambo ambalo ni wazi kaelewa uwezo wake lakini hata usajili huo umeonyesha malengo yake,” kilisema chanzo hicho.
Musa Mateja na Leen Essau, Dar es Salaam