
KATIKA hali ya kushangaza, mchungaji wa kanisa moja kutoka eneo la Mitaboni, Machakos nchini Kenya amelazimika kuwahonga walevi kwa kuwanunulia pombe ili wasifichue siri yake ya kuwatongoza na kuchepuka na wake wa watu.
Taarifa zinaeleza kwamba mchungaji huyo anapokea hela nyingi za sadaka na matoleo mengine ambayo yamemfanya kuwa tajiri na kutokana na hilo alishindwa kustahimili majaribu ya mwili na anasa za dunia.
“Pasta alikuwa ndumilakuwili. Jumapili anajifanya mtakatifu kanisani na siku zingine anakuwa mtu wa anasa za dunia,” alisema mmoja wa watu wake wa karibu ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Taarifa zaidi zinaarifu kwamba licha ya pasta huyo kuchepuka na wake za watu, alikuwa akibugia mvinyo kupindukia badala ya kujistahi kama tu aliyetarajiwa kuwa kielelezo na mfano mwema katika jamii.
“Pasta alikuwa chui aliyevalia ngozi ya kondoo, amezoea kutembea na wake za watu sugu na ni mlevi kupindukia,” jamaa huyo alidokeza.
Hata hivyo, ilifika siku ambapo walevi walichoshwa na mienendo ya pasta ya kupita na wake za watu bila aibu wala kujiheshimu. Walevi hao walikata kauli na kuamua kumkabili na kutisha kuanika uozo wake kwa waumini na pia kwa waume wa wanawake hao.
“Hata huoni haya kuchepuka na wanawake za watu licha ya kwamba unabugia pombe bila kuogopa chochote? Hujui kuwa tunaweza kuanika siri zako kwa watu na upoteze heshima yako? Tabia yako mbaya sana na imetushinda!” mlevi mmoja aliwaka huku akimtishia mtumishi huyo.
Pasta alipohisi mambo yamekuwa mabaya alianza kuwasihi walevi hao. “Jameni msichome picha. Mimi ni binadamu kama nyinyi na nina hisia za kimwili pia. Semeni mnachotaka ili msinichafulie jina mitaani,” mchungaji alisema.
Taarifa zinaarifu kwamba walevi hao kwa kauli moja walimuamuru kuwanunulia pombe hadi watosheke naye akakubali huku akiwasihi wasijaribu kumuanika. Hata hivyo baadhi yao baada ya kutosheka walisimama na kuanza kuondoka mmoja baada ya mwingine huku wakiimba nyimbo za kumsifu mchungaji huyo.
Duru zinaarifu kwamba pasta amekuwa kipenzi cha walevi hao na kila mara huwa anawanunulia dozi ili wasije wakaropoka na kumuanika.