
SEHEMU ya wanahabari nchini wamepewa semina juu ya uelewa wa mradi wa bomba la Mafuta Ghafi la Uganda–Tanzania, linalojulikana pia kama Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki linakusudia kusafirisha mafuta yasiyosafishwa kutoka Uganda kwenda Bandari ya Tanga, Tanzania, kwenye Bahari ya Hindi.

Semina hiyo iliyoandaliwa na mdau wa habari, Deogratius Kishombo na kuendeshwa na Mwanahabari Mwandamizi, Mwanasiasa na Mchumi, Dkt Prince Bagenda imedhaminiwa na Shirika Uwakala wa Meli nchini TASAC.

Akizungumza kwenye semina hiyo, Dkt. Prince Bagenda alisema kwakuwa mradi huu unahusisha nchi hizi mbili ni muhimu wanahabari hapa nchini kuwa na uelewa mpana juu ya mradi huu.

Amesema kwakuwa wanahabari ndio kiunganishi cha mawasilino na wananchi hivyo watakapopewa uelewa wataweza kuwaelewesha wananchi vizuri na kujua fursa wanazoweza kuzipata kwenye mradi huo.
“Tumeonelewa tuanze kuwapa uelewa wanahabari wetu hapa nchini ili wapate uelewa na kuweza kuwaelewesha wananchi juu ya faida za mradi huu mkubwa ambao wanatakiwa kunufaika nao.
“Ni lazima wananchi wajue kama kuna fursa mbalimbali ambazo wao wanaweza kunufaika moja kwa moja pamoja na kunufaika kwa serikali”. Alisema Dkt. Prince Bagenda.
Naye muandaaji wa semina hiyo, Deogratius Kishombo amesema lengo la semina hiyo ni kuwapa uelewa wanahabari ili waweze kuielimisha vizuri jamii juu ya mradi huu ambao unatarajiwa kuwa mkombozi kwa wananchi wa nchi hizi mbili.
Mwanahabari Justin Damiani ambaye ni mmoja kati ya wanahabari waliohudhuria semina hiyo alisema ameshukuru kupata uelewa mpana juu ya mradi huo ambapo hapo awali kuna mambo mengi sana alikuwa hayafahamu lakini kupitia semina hiyo amepata uelewa mpana sana.