
MAMBO yamekuwa mambo kwa msanii mwingine mkali kunako Bongo Fleva, Leopard Luhanga almaarufu Poemz; staa anayetrendi kwa sasa kutokana na mambo anayoyafanya kwenye gemu ambapo anahusishwa kutua kwenye lebo mpya ya Next Level Music (NLM) ya msanii Rayvanny akichukua nafasi ya pili kwenye lebo hiyo baada ya Mac Voice.
Akifunguka na Gazeti la IJUMAA juu ya tetesi hizo, Poemz anasema kuwa, kwa sasa hawezi kuzungumza sana juu ya ishu hiyo ila mambo yatakapokuwa safi atazungumza.
“Sina mamlaka ya kuweza kuzungumza juu ya jambo hilo, lakini sina tatizo kusaini kwa msanii yeyote ambaye tunaendana kwa sababu ni biashara ambayo itakuwa na faida kwake na kwangu.
“Siyo Rayvanny tu, hata ingekuwa ni lebo nyingine nipo tayari,” anasema Poemz ambaye yupo mbioni kuachia kichupa kingine kipya kinachokwenda kwa jina la Basi Jidai.
Ili kujidhihirisha na taarifa za kusainiwa kwa msanii huyo, Gazeti la IJUMAA lilimvutia waya Rayvanny ambapo alisema kuwa, kwa sasa aulizwe juu ya Mac Voice, kama kuna mwingine atakuja baadaye.
Mbali na Basi Jidai, Poemz anakimbiza na nyimbo nyingine kibao kwenye YouTube zikiwemo Nasema na Wewe, Ongeza, Nitavumilia, Alele, Moto, Na Wewe na nyinginezo.