
NDUGU yangu, mafanikio siku zote yanakuja kutokana na wewe kujenga uwezo au nguvu ya kukusaidia kufanikiwa kila siku. Hapo nikiwa na maana ni muhimu kujua kila siku, unatakiwa kutengeneza nguvu fulani ya kukusaidia kufanikiwa hata katika kipindi ambacho unajiona kama vile umechoka.
Bila kutengeneza nguvu kubwa ya kuweza kukusaidia kufanikiwa moja kwa moja, uwe na uhakika kuna wakati utakwama kufika kule unakotaka kufika. Pengine unajiuliza nguvu hii utaipataje ya kukusaidia kufanikiwa ili na wewe uweze kuitumia na ikusaidie?
Tafuta nguvu yako kubwa inapatikana muda upi. Ni rahisi sana kujenga nguvu ya kukusaidia kufanikiwa katika maisha yako kila siku, ikiwa utajua nguvu hiyo kubwa ya kukusaidia kufanikiwa inapatikana muda upi. Ni lazima ujue nguvu hiyo unaipata asubuhi, mchana au jioni?
Kwa wengi ili waweze kufanya mambo kwa kishindo na mafanikio makubwa, masaa yao ya mwanzo ya asubuhi huyatumia sana kufanya vitu ambavyo vinawapa faida na mafanikio kwao kwanza.
Ni masaa ambayo hawana mchezo nayo. Ni masaa ambayo siyo wanayatumia kwenye mitandao ya kijamii. Ni masaa ambayo yametengwa binafsi kwa ajili yao.
Kwa nini hiyo iko hivyo? Ni kwa sababu asubuhi mara nyingi ni muda ambao unakuwa umetulia sana, hivyo ni rahisi kufanya mambo mengi wakati akili ina nguvu nyingi ya kukusaidia kukupeleka kwenye mafanikio.
Hata wewe ili uweze kutengeneza nguvu kubwa itakayokusaidia moja kwa moja kufanikiwa unalazimika kutafuta muda wako bora wa kukufanikisha. Kumbuka, nguvu yako kubwa ya mafanikio inapatikana kwa kujua ipo muda upi. Ukilijua hilo lifanyie kazi.
Anza na kidogo ulichonacho; ili upate nguvu kubwa itakayokusukuma kuweza kufikia mafanikio makubwa, unalazimika kuanza na kidogo. Kama ni biashara anza na mtaji wowote ulionao halafu baadae mtaji huo utauwa ukiongezeka siku hadi siku.
Kwa chochote kile unachoanza nacho hata kama ni kidogo sana ukikifanya kwa muda mrefu kinakuwa kikubwa na kinakupa nguvu kubwa ya kuweza kukusaidia kufanikiwa moja kwa moja.
Kipi kidogo ulichonacho unashindwa kuanza nacho? Kuanza na kidogo ulichonacho ni moja ya kanuni kubwa sana ya kimafanikio ambayo unaweza kuitumia na kukutengenezea nguvu kubwa ya kimafanikio kwako.
Jenga nidhamu kubwa sana; kama kweli umeamua kutengeneza nguvu kubwa ya kukusaidia kufanikiwa, nidhamu ni muhimu sana. Haijalishi unakutana na nini au dunia imegeuka chini juu, lazima ujenge nidhamu.
Katika kile kidogo ulichoanza nacho, ukikijengea nidhamu ya muda mrefu, utashangaa maisha yakibadilika na ukizidi kusogea kwenda mbele kimafanikio kuliko vile unavyofikiri.
Nidhamu ni msingi mkubwa sana wamafanikio makubwa na pia inakujengea nguvu kubwa ya kukusaidia kufanikiwa moja kwa moja hata kama kuna watu walikuita hujiwezi au umechoka.
Weka pembeni tabia zinazokukwamisha; sina shaka kabisa upo hapo ulipo kimaisha kwa sababau tu ya yatabia f’lanif’lani ambazo umezishikilia kwa muda mrefu na zimekufikisha hapo ulipo. Sasa ili ufanikiwe ziweke pembeni tabia hizo.
Hutaweza kutengeneza nguvu kubwa ya kukusaidia kufanikiwa kama kweli bado unaendelea kushikilia tabia fulani fulani hivi zinazokuzuia kufanikiwa moja kwa moja kwenye maisha yako.
Kama ni uvivu, uweke pembeni, kama ni kupoteza muda weka pembeni, kama kutokujifunza weka pembemni, kisha amua sasa kuchukua tabia zile zitakazo kusaidia kuweza kujenga nguvu ya kufanikiwa moja kwa moja.
Kwanza napenda kumshukuru Mungu kwa kila jambo katika maisha yangu ya kila siku, najua yapo mengi sana ambayo namkosea. Kwa maneno, matendo na hata kwa kushindwa kutimiza wajibu.
Lakini kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwingi wa rehema bado naipa nafasi ya kuweza kuzungumza na wewe. Tutende mema ndugu zangu.
Unachopaswa kujua ni kwamba, ugumu wa maisha anao kila mtu kulinga na uzito wake, kuna wengine wana hali ngumu zaidi, lakini kuna wale wenye ahueni.
Katika mafanikio yoyote yale yana changamoto nyingi zipo za mazingira, mtaji, ushauri au watu wanaokuzunguka.
Maeneo uliyopo yanaweza kuwa kigezo cha kukukatisha tamaa kwa namna moja au nyingine katika kufikia jambo fulani. Mazingira unayoishi ni magumu kufanya kile unachokita. Inawezekana umejaribu kila namna lakini bado ikashindikana basi ni vyema ukahama hilo eneo la kwenda eneo ambalo unahisi litakuwa mafanikio kwa kile unachokitaka. Angalizo wakati mwingine ni vyema ukatafuta fursa kulingana na eneo lako.
Wapo watu wengine wana maono au ndoto nzuri, lakini zinashindwa kufanikiwa kwa sababu wanakatishwa tamaa na watu ambao walishakata tamaa zamani kwenye mioyo yao.
Watu wanaoweza kukukatisha tamaa anaweza kuwa ndugu, rafiki au mpenzi wako. Ni vyema wakati unataka ushauri ukachagua mtu au watu wa kukushauri kuliko kuomba ushauri kwa mtu yeyote.
Inawezekana una mpenzi ambaye anakukatisha tamaa kwa sababu wewe una tatizo f’lani katika mwili wako. Labda pengine una ulemavu wa kitu f’lani, huna elimu, huna pesa, huna kitu chochote cha maana.
Usikubali kumpa nafasi mtu ambaye ameshakata tamaa siku nyingi, mtu ambaye ana amini kuwa mafanikio yako kwa baadhi ya watu.
Hupaswi kukatishwa tamaa na mwanadamu ambaye ana mapungufu kama wewe, anaumwa kama wewe, analala kama wewe, anahangaika kama wewe, anaugua kama wewe, anakata tamaa kama wewe, alifeli masomo kama wewe, hana kitu kama wewe, siku moja atakufa kama wewe.
Binadamu wengine unaweza kusema labda wamezaliwa kuja kuwamatisha tamaa wenzao yani kila jambo ukifanya umekosea, kila kitu ukisema ni kibaya, wewe mtu wa aina gani, hakuna jema kwako.
Mtu wa namna hiyo ni yule ambaye amefeli katika kufikiria, upeo wake umegota sehemu aamini kama unaweza kuleta maajabu kwa umaskini ulio nao, kwa elimu ndoto uliyonayo, kwa ushamba ulionao. Pigania ndoto zako, acha kusikiliza maneno ya watu ukitaka kuamini kuwa hawafai, wewe acha kutimiza ndoto zako usikie watakavyokusimanga lakini hakikisha umefikia uone kama hawajakusifia kiaina.
Nakutakia wiki njema na yenye mafanikio tele. Mungu akubariki!