×

Unending love 61

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.

Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna ananasa ujauzito lakini William anamruka futi mia moja.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila William kujua chochote na mipango ya wazazi wake kumtoa ujauzito kihalali kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yanamsumbua inafanikiwa lakini matatizo mengine ya figo yanazuka upya na kusababisha akalazwe.

Upande wa pili, Suleikha anazidi kumganda Jafet kama ruba na hatimaye wawili hao wanaingia rasmi kwenye uhusiano wa kimapenzi. Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Nimetumwa na Dean (mlezi wa wanachuo) kuja kukuita, amesema kuna dharura inabidi uwahi haraka iwezekanavyo,” Lazaro, mwanachuo aliyekuwa akisoma na Jafet, alimkurupusha kijana huyo aliyekuwa amepumzika kwenye chumba chake akiwa na Suleikha.

“Kuna nini tena?” Suleikha aliingilia kati mazungumzo lakini hakuna aliyekuwa na majibu, harakaharaka Jafet akajiandaa na kutoka. Huku nyuma Suleikha naye alijiandaa na kuwafuata, akiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichotokea.

“Jafet! Unamfahamu huyu mzee?” mlezi wa wanachuo alimuuliza Jafet alipoingia ofisini kwake, akageuka na kutazama sehemu aliyokuwa anaoneshwa, akapigwa na butwaa kubwa kukutana uso kwa uso na baba yake Anna.

“Ndiyo namfahamu, shikamoo baba,” alijibu Jafet na kumuamkia kwa adabu mzee huyo. Licha ya yote yaliyowahi kutokea, Jafet alishajiwekea nadhiri ndani ya moyo wake kwamba ataendelea kuwaheshimu wazazi wa Anna kwa moyo wake wote.

“Marahaba Jafet, habari za siku? Umenenepa sana, naona maisha ya chuo yamekupendeza,” alisema baba yake Anna, wote wakacheka kisha mlezi huyo wa wanachuo akaendelea kumwambia Jafet kwamba huyo alikuwa ni mgeni wake na alikuwa na mazungumzo naye. Jafet akatingisha kichwa kuonesha kukubaliana na alichokuwa anaambiwa.

Baba yake Anna aliinuka pale alipokuwa amekaa na kutoka na Jafet mpaka nje ambapo walienda moja kwa moja mpaka kwenye bustani nzuri za maua zilizokuwa ndani ya eneo la chuo hicho.

“Samahani kama nitakuwa nimekuharibia mipango yako, kuna mazungumzo ya muhimu nahitaji kuzungumza na wewe,” alisema baba yake Anna huku akimuonesha Jafet sehemu ya kukaa.

“Najua zimepita siku nyingi bila kuwa na mawasiliano yoyote kati yetu. Najua ni kwa kiasi gani uliumia kutenganishwa na Anna lakini ilikuwa ni lazima iwe hivyo. Nimekuja hapa nahitaji msaada wako,” alisema baba yake Anna huku akikaa vizuri. Jafet akashusha pumzi ndefu na kumtazama usoni, akionesha kuwa tayari kutoa msaada wowote atakaoombwa.

“Anna anaumwa sana, hivi tunavyoongea amelazwa hapo Hospitali ya Muhimbili na hali yake siyo nzuri. Ukiachilia mbali kuumwa, anasumbua sana anataka kukuona, muda wote analia kama mtoto mdogo, tafadhali niko chini ya miguu yako naomba twende pamoja ukamuone,” alisema baba yake Anna huku akionesha uso wa huzuni uliochanganyikana na aibu.

Kwa yote waliyomfanyia kijana huyo, Jafet hakutegemea kama ipo siku watamfuata na kuomba msaada kwake hata mara moja. Akabaki anajiuliza maswali mengi yasiyo na majibu, akashusha tena pumzi ndefu na kutingisha kichwa kama ishara ya kukubali kile alichoambiwa na baba yake Anna.

“Naomba nikajiandae basi, nakuja sasa hivi,” alisema Jafet na kuinuka, akiwa anaondoka akashangaa kugundua kwamba kumbe muda wote wakati wakizungumza, Suleikha alikuwa amejibanza karibu yao bila wenyewe kumuona, akisikiliza kila kilichokuwa kinazungumzwa.

“Suleikha!” Jafet alimuita kwa sauti ya chini huku akigeuka kumtazama baba yake Anna kama alimuona, akajiridhisha kwamba hakuwa na taarifa zozote juu ya uwepo wake eneo hilo.

“Nimekusikia! Nimesikia kila kitu mlichokuwa mnajadiliana. Nimegundua kuwa kumbe hunipendi ila unataka kunitumia tu kama daraja,” alisema msichana huyo huku akianza kuangua kilio.
“Hapana, siyo hivyo mpenzi wangu, naomba uniamini.”
“Siwezi kukuamini Jafet, inaonekana bado mnapendana.”
“Kwa nini unasema hivyo Suleikha.”
“Nimemsikia baba yake anamuombea msamaha kwako, nimesikia,” alisema Suleikha huku akianza kulia, jambo lililompa wakati mgumu Jafet, ikabidi amshike mkono msichana huyo na kuondoka naye mpaka kwenye chumba chake ambapo alianza kumfafanulia kila kitu na kumtaka kama hamuamini, waongozane pamoja mpaka alikolazwa, wazo ambalo Suleikha alilipokea kwa mikono miwili.
Hakuna jambo lililokuwa likimsumbua msichana huyo moyoni mwake kama wivu mkali wa kimapenzi aliokuwa nao kwa Jafet. Alitamani ammiliki peke yake na asiwepo mwanamke yeyote wa kummendea.
Harakaharaka wawili hao walijiandaa na kurudi mpaka pale baba yake Anna alipokuwa amekaa. Jafet akamtambulisha Suleikha kama rafiki yake mkubwa na pia mwanachuo mwenzake, utambulisho ambao msichana huyo hakuridhika nao.
“Tumepanga tukimaliza chuo tufunge ndoa, nampenda sana Jafet,” alisema Suleikha na kumfanya baba yake Anna akose majibu. Wakaondoka na kuanza kuelekea Hospitali ya Muhimbili ambayo haikuwa mbali na chuo hicho.
Japokuwa muda wa kuwaona wagonjwa haukuwa umefika lakini kwa kuwa Anna alikuwa amelazwa kwenye wodi maalum ya VIP, hakukuwa na kipingamizi chochote, wakapita getini na kwenda moja kwa moja mpaka wodini.
“Nisubirini kwanza hapahapa nje,” alisema baba yake Anna na kumtaka Jafet na Suleikha wasimame mlangoni kwanza, yeye akaingia mpaka wodini ambako alimkuta mkewe akiwa anamnywesha juisi mgonjwa.
“Anna, nimekuja na sapraizi ambayo naamini utaipenda,” alisema baba yake Anna na kumfanya mkewe aache kumnywesha juisi mgonjwa, wote wakawa na shauku kubwa ya kutaka kujua ni sapraizi gani aliyokuja nayo.
Wakiwa katika hali hiyo, baba Anna alitoa ishara kwa Jafet na Suleikha waliokuwa nje, mlango ukafunguliwa kisha wakaingia, Jafet akiwa mbele huku Suleikha akimfuatia kwa nyuma.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

Leave a Comment