
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassana ameagiza miradi 49 iliyokutwa na kasoro wakati wa kukimbiza mwenge ichunguzwe na watu wote waliohusika wachukuliwe hatua mara moja.
Mhe. Samia ametoa maagizo hayo leo Alhamisi, Oktoba 14, 2021 wakati wa hafla ya kilele ha mwenge wa uhuru pamoja na kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Uwanja wa Magufuli, Chato mkoani Geita.
“Kabla ya kuja hapa (Chato) baadhi yetu tumepata fursa ya kushiriki ibaada maalum ya kumuombea Baba wa Taifa na aliyekuwa Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na viongozi wengine wa kitaifa kwa ujumla wao.
“Nawapongeza wananchi wa Chato kwa kuwa wenyeji wa Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu 2021 na kufanikisha kilele cha mbio hizi.
“Niwatake viongozi, tunapozima Mwenge mwakani idadi ya miradi yenye dosari ipungue sana, na kwa ile mikoa ambayo bado itajitokeza ina miradi yenye dosari tutaelewana wakati huo, hili ni onyo kwa wakuu wa mikoa na wilaya na wakurugenzi.
“Nimepewa taarifa kwamba ulinzi na usalama na mipaka ya nchi yetu iko imara na salama, navishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimamia vizuri amani na utulivu wa nchi yetu na mipaka yake.
“Miradi 49 imebainika kuwa na kasoro wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru hivyo naagiza wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu huu wachukuliwe hatua.
“Bila afya bora hatuwezi kuimarisha uchumi wetu, nchi yetu inakabiliwa na changamoto ya maradhi yasiyo ya kuambukiza kama Shinikizo la Damu. Natoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia ushauri wa kitaalum,” amesema Rais Samia.