×

Rais Samia, Mbunge Kibiti Wamwaga Misaada ya Kimaendeleo Mjawa, Kibiti

MBUNGE wa Kibiti, Twaha Mpembenwe akizungumza na wananchi wa Kata ya Mjawa wikiendi iliyopita.

 

 

Wakazi wa Kata ya Mjawa iliyopo Kibiti mkoani Pwani wameangukiwa na neema ya kimaendeleo kufuatia misaada inayoendelea kutolewa kwenye jimbo hilo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa jimbo hilo, Twaha Mpembenwe.

Sehemu wa umati uliofurika kwenye mkutano huo.

 

 

Akizungumza kwenye mkutano wa kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kumchagua kuwa mwakilishi wao bungeni, mbunge Mpembenwe aliwatajia misaada mbalimbali aliyogawa kwenye Kata hiyo ikiwemo misaada ya jumla kwenye jimbo hilo iliyowezeshwa na Rais Samia Suluhu.

Ofisi ya awali ya Mtendaji Kata ya Mjawa, Kibiti, Pwani.

 

 

Akitaja misaada hiyo Mheshimiwa Mpembenwe amewaambia wananchi hao kuwa kwenye kata hiyo ya Mjawa amegawa mifuko ya saruji 350 ambapo mifuko 50 amemkabidhi diwani wa kata hiyo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya mtendaji wa kata hiyo.

Ofisi mpya ya  Mtendaji Kata ya Kibiti inayojengwa na wananchi kwa kushirikiana na Mbunge Mpembenwe ambaye wiki iliyopita aliichangia mifuko 50 ya saruji.

 

 

Ameendelea kusema kuwa mifuko mingine 300 ameitoa kwenye kata hiyo kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Mjawa na Zahanati ya Motomoto ambazo ujenzi wake ulikuwa ukisuasua kwa muda mrefu na kusababisha kinamama kukosa sehemu salama ya kujifungulia kwenye kata hiyo pamoja na kukosa huduma nyingine za afya eneo hilo.

Katibu Mwenezi CCM Wilaya ya Kibiti, Suleiman Ndumbogani akiwasalimia wananchi waliohudhuria mkutano huo.

 

 

Kauli hiyo ilipokelewa kwa vifijo na nderemo na umati uliofurika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata hiyo.

Wanachi wa Jaribu Mpakani Kata ya Mjawa wakimpongeza Mheshimiwa Mpembenwe kwa misaada ya ujenzi wa Zahanati, Shule na ofisi ya chama.

 

 

Upande wa elimu Mheshimiwa Mpembenwe amesema amegawa mifuko 350 ya saruji, mabati 50 na nondo tani moja kwa ajili ya maboresho ya Sekondari ya Mwambao.

Burudani ya ngoma za asili nayo ilinogesha mkutano huo.

 

 

Akielezea suala la maboresho ya sekondari hiyo Mheshimiwa Mpembenwe amesema lengo lake ni kuhakikisha wanafunzi kwenye kata hiyo wanasoma katika mazingira bora ili waweze kufanya vizuri na kutokomeza ziro kwenye jimbo hilo na kuingia kwenye ushindani wa kushika nafasi za juu kitaifa.

Mbunge Mpembenwe (katikati) akipokea saruji kutoka kwa washirika wake Benki ya NBC hivi karibuni kwaajili ya kuendeleza harakati za kimaendeleo jimboni kwake.

 

 

“Ili watoto wetu waweze kufanya vizuri ni lazima tuwajengee shule za kisasa ili wasome katika mazingira bora yatakayowashawishi kufanya vizuri na kuingia kwenye ushindani wa kufanya vizuri kitaifa” alisema Mheshimiwa Mpembenwe.

HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS NA ISSA MNALLY /GPL

Leave a Comment